Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta. Picha ya maktaba
Dar es salaam.
Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta amesema anasubiri kukamilika kwa utaratibu wa CCM wa kugombea urais ili aingie rasmi kwenye mbio hizo kwa kuwa anaridhika na mambo matatu ambayo anasema yanamfanya ashawishike kugombea nafasi hiyo ya juu katika siasa nchini.
Sitta, mwanasiasa mkongwe na Spika wa Bunge la Tisa, ni mmoja kati ya makada wa chama hicho tawala wanaotarajiwa kuchukua fomu za kuomba ridhaa ya CCM kugombea urais kumrithi Jakaya Kikwete, ambaye anamaliza vipindi vyake viwili vya urais Oktoba mwaka huu.
Akizungumza na Mwananchi mwishoni mwa wiki, Sitta alisema zaidi ya mambo hayo matatu, anaamini ana ushawishi mkubwa na Watanzania wengi wanamwamini katika utendaji kazi wake.
“Nina mengi nimefanya kutokana na historia yangu ya kiutendaji na ndiyo nitakayoitumia kama mtaji utakaonibeba kwenye harakati hizi,” alisema.
Sitta, ambaye alikuwa mwenyekiti wa Bunge la Katiba, alitaja mambo hayo matatu ambayo ni mtaji wake kuwa ni uendeshaji wake wa chombo hicho cha kuandika Katiba, uendeshaji wake wa Bunge na uzoefu wake wa muda mrefu kwenye nafasi mbalimbali alizowahi kushika.
Sitta, ambaye alikuwa mwenyekiti wa Bunge la Katiba, alitaja mambo hayo matatu ambayo ni mtaji wake kuwa ni uendeshaji wake wa chombo hicho cha kuandika Katiba, uendeshaji wake wa Bunge na uzoefu wake wa muda mrefu kwenye nafasi mbalimbali alizowahi kushika.
“Niliendesha Bunge la Katiba kwa mafanikio na hata kupatikana kwa Katiba Inayopendekezwa,” alisema Sitta.
“Watanzania wataangalia wenyewe historia yangu kwani mimi ndiye mwenyekiti niliyefanikisha kutimiza ndoto za Watanzania kupata Katiba mpya kupitia Bunge Maalumu la Katiba, haikuwa rahisi katika tukio hilo,” alisema.
Hata hivyo, Bunge la Katiba halikuisha kwa maridhiano baada ya wajumbe kutoka vyama vinne vya Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD kususia vikao kwa madai kuwa chombo hicho kiliweka pembeni Rasimu ya Katiba iliyokuwa na maoni ya wananchi.
Juhudi za Sitta kuwarejesha vikaoni ziligonga mwamba, lakini mchakato ukaendelea hadi Katiba Inayopendekezwa ilipopatikana.
Sitta alisema mtaji wake mwingine katika mbio za urais ni na kuimarisha demokrasia ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano.
“Mimi ndiye niliyebadilisha Bunge baada ya kubadilisha kanuni za Bunge mwaka 2007, ambazo zilitoa uhuru, haki na usawa kwa wabunge wote bila kujali wapinzani,” alijigamba.“Bunge langu ndilo liliibua umaarufu wa wapinzani na ndipo wakaibuka akina Zitto Kabwe na Dk Wilbroad Slaa kwani walipata nafasi ya kuibua hoja na kuhoji udhaifu wowote wa Serikali.”
Sitta alisema haikuwa rahisi kufanya mabadiliko hayo kwani baadhi ya wanachama wenzake walipingana na jambo hilo, lakini alilisimamia kama Spika na kulipeleka bungeni.
“Nilipingwa sana lakini nikasema hapana, kuna Tunu za Taifa zilizokuwa zimeharibiwa na lazima tuzirejeshe na matokeo yake kwa sasa yameanza kuonekana,” alisema.
“Hata katibu mkuu wetu wa CCM, Abdurahman Kinana ambaye anakosoa Serikali na kuagiza uwajibikaji, siyo kuwaachia wapinzani tu, anayaona na anasema kwa kuwa wanaofanya hayo yanayoonekana ni watu wetu ndani ya CCM,” alisema Sitta.
Alisema jambo la tatu ni uzoefu wake katika utawala kuanzia awamu ya kwanza hadi sasa.
“Nimefanya kazi na marais wa awamu zote, wananikubali kwa kuwa mimi ni mchapakazi. Wasingekuwa wananichukua kama si mchapa kazi,” alisema Sitta ambaye ana umri wa miaka 73.
Lakini, mbunge huyo wa Urambo Mashariki alisema kwa sasa Taifa lipo kwenye kipindi kigumu.
“Katika kipindi hiki, lazima Watanzania wachuje na waangalie ni kiongozi gani atakayewafaa katika uongozi ujao na si kukurupuka na kudanganywa,” alisema.
Sitta pia aligusia mgogoro uliopo baina ya Serikali na viongozi wa dini kuhusu Katiba Inayopendekezwa, akisema ni makosa kwa viongozi hao wa kiroho kuingilia masuala la kisiasa.
Alisema si kila kilichohitajika kuingia kwenye Katiba, kingepita sasa.
“Mazuri na mambo yote ya msingi yameingizwa kwenye Katiba hiyo na siyo rahisi kulazimisha maoni ya kila mtu yaingie, wasubiri labda kwa kipindi kijacho yataingia,” alisema.
Viongozi wa Jukwaa la Wakristo wameagiza waumini wao waikatae Katiba Inayopendekezwa wakidai Serikali iliahidi kuingiza suala la Mahakama ya Kadhi kwenye Katiba ili Waislamu wakubali kuipitisha, jambo ambalo linachukuliwa kuwa ni kuingilia masuala ya kisiasa.
|
0 Comments