Maandamano ya kupinga ghasia dhidi ya wageni yalifanyika mjini Durban.
Raia wa kigeni wakitoa bidhaa katika maduka yao kufuatia kushambuliwa na wenyeji.
Wapinga wahamiaji hayo wakikimbia baada ya kurushiwa mabomu ya machozi.Raia wa kigeni wakiamua kujihami kwa kuchukua silaha kupambana na wenyeji.Baaadhi ya raia ya kigeni wakiwa wamehifadhiwa katika kambi baada ya kukimbia fujo na kuepusha maisha yao.
Nchi jirani na Afrika Kusini zimeanza matayarisho ya kuwaondoa raia wao kutoka nchi hiyo wakati Umoja wa Mataifa ukieleza wasi wasi wake mkubwa kutokana na mashambulio hayo ya chuki dhidi ya wageni .
Mashambulio ambayo yamesababisha maelfu ya watu kukimbia makaazi yao.

Ghasia hizo dhidi ya wageni, ambazo zilianzia katika mji wa mashariki wenye bandari wa Durban, zimesababisha kiasi cha watu sita kuuwawa na kusambaa hadi katika mji wa kibiashara wa Johannesburg.
"Nchini Afrika Kusini, mashambulizi ya chuki dhidi ya wageni katika muda wa wiki tatu zilizopita, yamesababisha watu zaidi ya 5,000 raia wa kigeni kukimbia makaazi yao," lilisema shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwahudumia Wakimbizi (UNHCR) na kuongeza kuwa lina "wasi wasi mkubwa".
"Tungependa kusisitiza kwamba wale walioathirika katika mashambulizi haya ya hisia za chuki kwa wageni ni wakimbizi na wale wanaotaka hifadhi ambao wamelazimika kukimbia nchi zao kutokana na vita na kusakwa na serikali zao, " UNHCR imesema.
Makambi ya muda
Raia hao wa kigeni wanajihifadhi sasa katika makambi ya muda.
Nchi jirani ya Zimbabwe, Malawi na Msumbiji zimetangaza mipango ya kuwarejesha nyumbani raia wao, wakati ghasia hizo zimesababisha hasira miongoni mwa nchi za eneo hilo.
Balozi wa Zimbabwe nchini Afrika kusini, Isaac Moyo amesema hatua ya kuwarejesha nyumbani kiasi ya Wazimbabwe 1,000 kutoka Durban itaanza Jumapili (19.04.2015).
Katika mji mkuu wa Zimbabwe, Harare , waandamanaji walipita katika ubalozi wa Afrika kusini wakishutumu kile walichokiita "mauaji ya kiwendawazinmu na ya kikatili" ya Waafrika wenzao.
Nchini Msumbiji , kundi la watu wapatao 200 jana Ijumaa lilizuwia kivuko cha mpakani cha Lebombo kuelekea nchini Afrika kusini , wakiyapiga mawe magari ya Afrika kusini.
"Waandamanaji walizuwia barabara kwa muda wa nusu saa , wakikataa kuruhusu magari yenye namba za Afrika kusini kupita" kamanda wa polisi wilayani Moamba Alfonso Rocco ameliambia shirika la habari la AFP.
Radio yasitisha kupiga muziki wa Afrika kusini
Nchini Zambia , radio ya binafsi imesitisha kupiga muziki kutoka Afrika kusini wakipinga mashambulizi hayo ya chuki kwa wageni.
"Radio QFM imeacha kabisa kupiga muziki wa Afrika kusini kuanzia leo, Aprili 17 kupinga mashambulizi dhidi ya wageni yanayotokea nchini humo," Mkurugenzi mtendaji wa QFM Asan Nyama amesema katika taarifa iliyowekwa katika tovuti ya kituo hicho cha redio.
Mwimbaji wa Afrika kusini Kelly Khumalo alilazimika kuahirisha tamasha lake la muziki mjini London kwasababu ya hasira , wakati Big Nuz -- kundi ambalo hupiga muziki maarufu ujulikanao kama Kwaito -- lilibidi kufuta tamasha la muziki nchini Zimbabwe, waziri katika ofisi ya rais Jeff radebe amesema siku ya Ijumaa.
Hasira katika nchi jirani imeongezwa na ukweli kwamba nchi hizo zimewahifadhi maelfu ya Wafrika kusini waliokimbia nchi zao wakati wa mapambano dhidi ya utawala wa kibaguzi--suala ambalo rais Jacob Zuma amelisema katika hotuba katika bunge siku ya Alhamis.
"Tulihifadhiwa kwa ukarimu mkubwa , utu na heshima na ndugu zetu katika bara zima," Zuma amesema, akidokeza kwamba mshikamano wao ulikuwa muhimu kuweza kufanikisha uhuru na demokrasia ambayo hivi sasa tunafaidi".
Mfalme ndio chanzo cha ghasia
Ghasia za hivi karibuni zinalalamikiwa kwamba zimetokea kwa kiasi kikubwa kutokana na hotuba mwezi uliopita iliyotolewa na mfalme Goodwill Zwelithini, kiongozi wa kabila la Wazulu , ambae amelaumu wageni kutokana na kiwango cha juu cha uhalifu nchini Afrika kusini na kusema ni lazima "wafungashe mizigo yao na kuondoka ".
Mfalme huyo amesema kuwa maneno yake yametafsiriwa vibaya , lakini baadhi wanasema, Zwelithini anasema kile ambacho wengi wanakihisi.
Uchumi wa Afrika kusini unawavutia wahamiaji wengi wale wanaoingia nchini humo kihalali na wale wanaoingia pia kinyume na sheria , lakini hali ya kutokuwa na usawa pamoja na ukosefu mkubwa wa ajira miongoni mwa raia wa nchi hiyo kunajenga hali ya kutowapenda wageni.
Jumuiya ya Kiuchumi ya Mataifa ya Afrika Magharibi (ECOWAS) imeshutumu "mauaji ya kinyama, kihalifu na yenye chuki dhidi ya wageni yanayofanywa kwa raia wa kigeni wasio na hatia", na kuitaka serikali ya Afrika Kusini kuchukua hatua haraka kusitisha ghasia hizo.
NA DW
Mwandishi: Sekione Kitojo/afpe