Polisi nchini Afrika Kusini akituliza ghasia baada ya shambulizi kwenye maduka ya raia wa kigeni nchini humo.
Raia wawili wa Somalia wamenusulika kuuwawa baada ya kuchomwa moto nchini Afrika Kusini wakati wa wimbi la mashambulizi yanayolenga raia wa kigeni. Maduka kadhaa ya Wasomali pia yamechomwa moto na kuteketezwa kabisa.

Jeshi la Polisi nchini Afrika Kusini limesema kuwa raia hao wa Somalia wamenusulika kuuawa baada ya kuchomwa moto wakiwa madukani mwao katika kitongoji cha Umlazi Kusini mwa Jiji la Durban, na wamekimbizwa hospitali kwa ajili ya matibabu.
Polisi imeongeza pia kuwa watu 17 wametiwa nguvuni katika machafuko yanayoendelea katika Mji wa Durban. Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini Afrika Kusini, Thulani Zwane amesema hali bado ni tete katika maeneo yaliyoathiriwa na wimbi la kuwashambulia raia wa kigeni nchini humo na kwamba jeshi hilo linafanya juhudi za kudhibiti hali hiyo.
Machafuko hayo yalianza wiki mbili zilizopita baada ya wakazi wa vitongoji vya Isipingo na Chatsworth kuvamia, kuiba na kuharibu maduka ya raia wa kigeni.
Zaidi ya raia elfu moja wa kigeni wamekimbia nyumba zao katika mji wa Durban kwa kuhofia mashambulizi ya wenyeji.