APRILI 13, 1922 Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alizaliwa katika Kijiji cha Butiama, Wilaya ya Musoma, mkoa wa Mara, Tanzania (wakati ule: Tanganyika).
Alikuwa mmojawapo kati ya watoto 26 wa Nyerere Burito, chifu wa kabila la Wazanaki.
Alipokuwa mtoto Nyerere alichunga mifugo ya baba yake; katika umri wa miaka 12 alianza shule ya msingi akitembea kilomita 30 hadi Musoma.
Baada ya kumaliza shule ya msingi aliendelea kusomea shule ya wamisionari Wakatoliki huko Tabora.
Katika umri wa miaka 20 alibatizwa akawa Mkristo Mkatoliki hadi mwisho wa maisha yake.
Baada ya kufaulu vizuri alienda kusomea ualimu huko Makerere, Kampala, Uganda kuanzia mwaka 1943 hadi 1945.
Akiwa Makerere alianzisha tawi la Umoja wa Wanafunzi Watanganyika, pia alijihusisha na tawi la Tanganyika African Association (TAA).
Baada ya kumaliza masomo ya ualimu alirudi Tabora akifundisha shule ya St.Mary.
Mwaka 1949 alipata nafasi ya kwenda kusoma kwenye Chuo Kikuu cha Edinburgh, Scotland ambapo alipata M.A. ya historia na uchumi (alikuwa Mtanganyika wa kwanza kusoma katika chuo kikuu cha Uingereza na wa pili kupata shahada ya elimu ya juu nje ya Tanganyika).
Aliporejea kutoka masomoni, alifundisha Historia, Kiingereza na Kiswahili katika shule ya St. Francis.
Mwaka 1953 alichaguliwa kuwa rais wa chama cha Tanganyika African Association (TAA), chama ambacho alikisaidia kukijenga alipokuwa mwanafunzi katika chuo kikuu cha Makerere.
Mwaka 1954 alibadilisha jina la chama cha TAA kwenda chama cha Tanganyika African National Union (TANU), ambacho pia kilikuwa cha kisiasa zaidi kuliko TAA. Ndani ya mwaka mmoja chama cha TANU kikawa tayari chama cha siasa kinachoongoza nchini Tanganyika.
Uwezo wa Nyerere uliwashtua viongozi wa kikoloni akalazimika kuchagua kati ya siasa na kazi ya ualimu. Nyerere alisikika akijisemea kuwa mwalimu kwa kuchagua na mwanasiasa kwa bahati mbaya.
Alijiuzulu ualimu na kuzunguka nchi nzima ya Tanganyika kuzungumza na watu wa kawaida na machifu ili kuleta umoja katika kupigania uhuru. Pia alizungumza kwa niaba ya TANU katika Trusteeship Council na Fourth Committee ya Umoja wa Mataifa (UN) huko New York.
Uwezo wake wa kuongea na wa kuunganisha watu ulimwezesha kufanikisha Tanganyika kupata uhuru bila umwagaji wa damu.
Ushirikiano mzuri aliouonyesha aliyekuwa gavana wa wakati huo, Richard Turnbull, ulisaidia pia kuharakisha upatikanaji wa uhuru.
Nyerere aliingia katika bunge la kikoloni mwaka 1958 na kuchaguliwa kuwa waziri mkuu mwaka 1960.
Mwaka 1961 Tanganyika ilipata uhuru wake na tarehe 9 Desemba 1961 Nyerere alichaguliwa kuwa waziri mkuu wa Tanganyika huru; mwaka mmoja baadaye akawa rais wa kwanza wa Jamhuri ya Tanganyika.
Nyerere alikuwa kiungo muhimu katika muungano wa Tanganyika na Zanzibar kutengeneza Tanzania mara baada ya mapinduzi ya Zanzibar mwaka 1964 yaliyomtoa madarakani sultani wa Zanzibar Jamshid bin Abdullah.
Tarehe 5 Februari 1977 aliongoza chama cha TANU kuungana na chama tawala cha Zanzibar Afro Shirazi Party na kuanzisha chama kipya cha CCM (Chama cha Mapinduzi) akiwa mwenyekiti wake wa kwanza.
Nyerere aliendelea kuongoza taifa hadi 1985 alipomwachia nafasi rais wa pili, Ali Hassan Mwinyi.
Hata hivyo aliendelea kuongoza CCM hadi mwaka 1990 na kuwa na athari kubwa katika siasa ya Tanzania hadi kifo chake.
Nyerere alikaa muda mwingi kwake Butiama akilima shamba lake. Pamoja na haya alianzisha taasisi yenye jina lake; mwaka 1996 alionekana akiwa mpatanishi wa pande mbalimbali za vita vya wenyewe kwa wenyewe huko Burundi.
Tarehe 14 Oktoba 1999 aliaga dunia katika hospitali ya St Thomas mjini London baada ya kupambana na kansa ya damu.
0 Comments