Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akitoa machozi wakati John Magufuli akitangazwa kuwa mgombea wa CCM
WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda, alimwaga chozi ndani ya mkutano mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kulilia urais.
Majina matano ya wasaka urais kupitia CCM, yaliyowasilishwa Kamati Kuu (CC) ya chama hicho, ni January Makamba, Membe, Dk. Asha-Rose Migiro, Balozi Salum Ali na John Magufuli.
Taarifa zinasema, majina hayo yalipatikana kabla ya vikao vya chama vilivyofanyika ili kumbeba mmoja wa wagombea wa nafasi hiyo.
Mkutano mkuu wa CCM ulioteuwa mgombea wake urais, ulianza Jumapili iliyopita na kumalizika siku iliyofuata – Jumatatu,13 Julai 2015. John Pombe Magufuli, ndiye aliyeibuka mshindi miongoni mwa wagombea 38 waliojitokeza kuomba nafasi hiyo.
Taarifa kutoka makao madogo ya CCM, Lumumba na Ikulu zinasema, majina hayo matano yalichongwa kwa ustadi mkubwa na watu kutoka Idara ya Usalama ya CCM ili kumnufaisha, Bernard Membe, mmoja wa walioapa kusaka urais kufa na kupona.
Pinda hakupatikana kueleza kwa undani kilichosabisha kumwaga chozi hadharani.
Hata hivyo, wachambuzi wa mambo ya kisiasa wanasema, kilichomliza Pinda, ni hatua ya Kikwete ya kumchinja katika hatua za awali, wakati alikuwa na sifa zote za kufikishwa Halmashari Kuu ya taifa (NEC) ya chama hicho.
Habari zinasema, kabla ya kuchukua fomu, Pinda alikutana na Rais Jakaya Kikwete ili kuomba ridhaa ya kugombea nafasi hiyo. Kikwete aliridhia suala hilo.
“Pamoja na kwamba Kikwete aliombwa na watu wengi, lakini ilitegemewa kwa kuwa Pinda ni mmoja wa wasaidizi wake, basi angehakikisha kuwa anampitisha na kumuingia NEC,” anaeleza mchambuzi wa masuala ya kisiasa, Kondo Tutindaga.
Msaidizi mwingine wa Kikwete ambaye alikuwa mmoja wa wagombea urais na ambaye jina lake liliondolewa katika hatua za awali, ni Dk. Mohammed Gharib Bilal, makamu wa rais wa Jamhuri.
Anasema, “…uzito wa hoja yangu umejikita katika msingi mmoja. Kwamba, viongozi hawa wawili (Pinda na Bilal), walitakiwa wapigiwe kura ama katika CC au NEC.
“Ilitakiwa washindwe kwa kura kidemokrasia, kuliko kutupwa na kamati ya maadili na hivyo kushindwa kuingia katika watano bora,” anaeleza.
Anaongeza, “kwangu mimi, ilikuwa bora hata kubadili kanuni ili kuongeza wigo wa idadi ya wagombea kuliko kulazimika kuwaacha watu ambao ni msingi wa umoja wa taifa, ikulu yetu na chama tawala.”
Anasema, “watu wanajiuliza. Inakuwaje tunakuwa na waziri mkuu, makamu wa rais na jaji mkuu mstaafu ambao wana mapungufu makubwa yasiyoruhusu kupigiwa kura mbele ya vikao vya chama?”
Pinda aliyekuwa ameapa kufia katika mbio za urais, jina lake liliondolewa katika hatua za awali za kinyang’anyiro hicho.
0 Comments