CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kwa ushirikiano wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), wamezindua kampeni zao pamoja na Ilani ya uchaguzi, huku wakitaja vipaumbele vitano watakavyovisimamia endapo watapewa ridhaa ya kuongoza nchi.
Uzinduzi huo ulifanyika jana Dar es Salaam katika viwanja vya Jangwani huku maelfu ya wananchi na wafuasi wa vyama vinavyounda Ukawa, wakiwa wamefurika kusikiliza hotuba na sera za wagombea wa nafasi ya urais, makamu na nafasi ya urais wa Zanzibar.
Katika hotuba yake ya takribani dakika 10, mgombea wa nafasi ya urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa, alitaja vipaumbele vyake vitano ambavyo ni elimu, kilimo, afya, mawasiliano na biashara, kisha akaomba kura kwa wananchi.

Akizungumzia kwa ufupi vipaumbele hivyo, Lowassa aliyefuatana na mgombea mwenza, Juma Haji Duni pamoja na mgombea wa urais Zanzibar, Seif Sharif Hamad, alisema kipaumbele cha kwanza ni elimu.
Akifafanua kipeumbele hicho cha elimu alisema endapo ataingia madarakani elimu itakuwa bure kuanzia ngazi ya elimu ya msingi hadi chuo kikuu na kwamba uwezo wa kufanya hivyo upo ikiwa rasilimali za nchi zitatumika vizuri.
Kuhusu kilimo alisema hicho ni kipaumbele kinachogusa wananchi wengi na kwamba atahakikisha kinaboreshwa hususan kutumika kwa benki ya kilimo ili iweze kuwahudumia wakulima vizuri na wao wanufaike na mazao yao badala ya mazao hayo kuoza kabla ya kufika sokoni na kupata bei bora.
Akizungumzia kipaumbe cha afya, Lowassa alisema ni jambo muhimu sana ambalo linapaswa kuangaliwa na kuboreshwa kwani hali ya huduma ya afya kwa sasa haipatikani kwa kiwango cha kuridhisha.
Kipaumbele cha nne alisema ni uimarishaji wa mawasiliano akifafanua kwamba dunia ya sasa ni ya sayansi na teknolojia na kwamba mawasiliano yanapaswa kuwa na kiwango kinachoridhisha ili kuwa na nchi yenye uchumi unaoimarika.
Aidha kuhusu kipaumbele cha biashara, mgombea huyo alisema iwapo Ukawa watashika dola, reli ya kati itaboreshwa akisema hakuna sababu ya kushindwa na nchi ndogo kama vile Rwanda ambayo imeboresha miundombinu yake pamoja na Malawi.
Alisisitiza kuwa mabadiliko yanahitaji nidhamu ya hali ya juu ila wapo wavivu ambao hawapendi kufanya kazi, na kwamba hao wanapaswa kubadilika na wasipoweza watashindwa kwenda na mabadiliko hayo.
“Mabadiliko yanahitaji nidhamu ya hali ya juu, ila wapo wavivu, inabidi wabadilike la sivyo watashindwa kwenda na mabadiliko,” alisema Lowassa.
Awali akizindua ilani ya uchaguzi watakayotumia endapo wataingia madarakani, Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe, alisema ilani hiyo ni ya Chadema lakini inaungwa mkono na vyama vyote vinavyounda Ukawa kutokana na kuwa viongozi wa vyama hivyo wameshiriki kutoa maoni yao ambayo yaliingizwa kwenye ilani hiyo.
Alisema ilani hiyo imebeba na kuzingatia maslahi mapana ya taifa, na kwamba umoja wao umetayarisha ilani ambayo ina sera rafiki kwa Watanzania wote bila kujali itikadi za vyama vyao.
Mbowe alisema Ukawa wanapozungumzia mabadiliko si kwa ajili ya kuiondoa CCM madarakani bali kubadili maisha ya Watanzania, akisema mabadiliko hayatakuwa na maana kwa wananchi kama wataendelea kubaki kuwa masikini.
“Tunataka mabadiliko yatakayowaletea wananchi maisha bora. Tunataka kuondoka kwenye umasikini kwa sababu umasikini ni laana. Ukawa hatutamani umasikini, tunatamani watu wote wawe na uwezo wa kuishi maisha bora,” alisema Mbowe.
Sumaye amtetea
Lowassa Awali akizungumza kabla ya Lowassa kutoa hotuba yake, Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye, aliyehama Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwenda Ukawa alitetea afya ya Lowassa.
Katika utetezi wake alisema Lowassa anasakamwa kuhusu ugonjwa wake na kusisitiza kuwa mtu yeyote aliyefikisha umri za zaidi ya miaka 50, ni lazima asumbuliwe na maradhi.
“Kwa mtu mwenye umri wa miaka 50 na kuendelea, hawezi kuwa mzima kwa asilimia 100, ni jambo la kawaida mbona viongozi wetu tunawashuhudia wakienda kutibiwa nje na kurejea, urais siyo kazi ya kubeba zege Ikulu,” alisema Sumaye.
Aliongeza kuwa cha msingi ambacho rais anatakiwa kuwa nacho ni timu imara ambayo ataipa majukumu ya kufanya na yeye aangalie utendaji wao.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia alivitaka vyama vyote vya siasa kufanya kampeni kwa kuzingatia sheria na kwamba wao Ukawa wanaleta matumaini kwa wananchi kwa kuhubiri umoja na kamwe hawatachochea vurugu.
Kwa upande wake, Duni alisema, endapo watafanikiwa kuingia madarakani moja ya jukumu lao la msingi ni kuhakikisha wanalinda heshima ya mwanamke kwa kuweka mazingira bora pamoja na huduma nzuri za afya kwa ajili ya wanawake.
Alisema jukumu kubwa ambalo watahakikisha wanatekeleza ni kulinda heshima ya mwanamke kwa kutengeneza mazingira bora pamoja na huduma nzuri za afya kwa ajili ya wanawake.
Kaimu Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Twaha Taslima alisema, wagombea hao wa Urais pamoja na Makamu wake ni viongozi wanaopendwa na wananchi wengi na wanajua matatizo ya wananchi hivyo hakuna shaka wako pamoja na wananchi wao.
Aidha, Mwenyekiti wa chama cha NLD, Dk Emmanuel Makaidi alisema, wanamichezo wote hawana budi kumchagua Lowassa ili aweze kuleta mabadiliko katika sekta ya michezo.