MSAJILI wa Hazina ametoa siku 30 kuanzia jana kwa wawekezaji wote walionunua viwanda na mashamba yaliyokuwa miliki ya serikali, kuwasilisha taarifa za sasa za utekelezaji wa masharti ya mikataba yao vinginevyo, serikali itarejesha umiliki wake.
Mbali na hilo, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imebatilisha miliki za ardhi za mashamba makubwa 29 na viwanja 10 katika mikoa saba nchini, kutokana na kukiukwa kwa masharti ya umiliki ardhi.

Agizo la Msajili huyo wa Hazina pamoja na hatua za Kamishna wa Ardhi zimekuja ikiwa ni wiki chache tangu Rais John Magufuli aapishwe kuwa Rais wa Awamu ya Tano wa Tanzania, ambaye katika kampeni za kuwania nafasi hiyo, aliahidi iwapo atashinda, atanyang’anya mashamba yote yaliyohodhiwa na watu bila kuendelezwa.
Awali, katika Mkutano wa Bunge wa Februari mwaka huu, aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi alitoa msimamo wa serikali na kusema mashamba yote makubwa ambayo hayajaendelezwa, yatataifishwa na mengine yatagawiwa kwa wananchi.
Kwa mujibu wa tangazo la agizo lililotolewa jana kwenye vyombo vya habari nchini, Msajili huyo wa Hazina, Lawrence Mafuru, hivi sasa ofisi yake inarejea mikataba yote ya mauzo wa viwanda na mashamba iliyoingiwa kupitia mpango wa ubinafsishaji.
Alisema mapitio hayo yanafanyika kwa sababu wapo wawekezaji waliokiuka masharti ya mikataba hiyo, ikiwa ni pamoja na kutoendeleza viwanda na mashamba kwa mujibu wa mikataba yao.
Pia alisema wapo wawekezaji waliouza mashine walizozikuta bila kurudisha mashine nyingine mbadala na wengine hawajakamilisha malipo ya ununuzi wa viwanda na mashamba pamoja na kubadilisha matumizi ya viwanda na mashamba bila idhini.
Kuhusu ubatilishwaji wa miliki za ardhi katika viwanja na mashamba hayo, Kamishna wa Ardhi wa wizara hiyo, Dk Moses Kusiluka, aliitaja mikoa hiyo saba ambayo hati za viwanja na mashamba yake yamebatilishwa umiliki wake kuwa ni pamoja na Dar es Salaam, Arusha, Morogoro, Lindi, Mbeya, Kilimanjaro na Tanga.
Dk Kusiluka alisema ubatilishaji wa miliki za ardhi kwenye mashamba na viwanja hivyo ulianza rasmi Oktoba 30, mwaka huu na aliyataja mashamba hayo kuwa ni pamoja na mashamba manane yaliyo kwenye wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro, ambayo ni shamba namba 108, 150, 185 na 79 yaliyopo eneo la Wami Luhindo.
Mengine ni shamba namba 132 lililopo eneo la Kifugame, Wami Luhindo, shamba namba 5, la Wami Valley, shamba namba 124 la Mlali na mashamba namba 195 na 196 yaliyopo Nguru ya Ndege.
Aidha, mashamba mengine tisa yaliyobatilishwa miliki zake za ardhi yapo mkoani Lindi katika maeneo mawili tofauti ambayo ni Kitunda yenye mashamba mawili namba 31035 na 12588.
Eneo la pili ni Kikwetu yenye mashamba saba, ambayo ni namba 6143, 7615, 5251, 6555, 2865, 13598 na 6070. Dk Kusiluka aliongeza kuwa Mkoa wa Arusha, Wilaya ya Monduli yapo mashamba 12, yaliyobatilishwa miliki zake na mashamba hayo yapo kwenye maeneo matatu ya Mswakini Juu, Lolkisale na Meserani.
Aliyataja mashamba yaliyopo eneo la Mswakini Juu kuwa ni shamba namba 2275, 2276, 2277, 2278 na eneo la Lolkisale ni shamba namba 13, 9, 76 na 2324. Eneo la Meserani ni shamba namba 169, 59, 171, 170.
Alisema ubatilisho wa miliki za ardhi ya mashamba hayo umefanywa kwa kuzingatia sheria za ardhi na mashamba hayo yalibatilishwa miliki zake kati la Mei hadi Oktoba mwaka huu. Aidha, viwanja 10 vilivyobatilishwa miliki zake ni viwanja vinne vilivyoko mkoani Mbeya.
Mchanganuo wake ni viwanja viwili vilivyo eneo la Forest vyenye namba 820 na 1112 kwenye kitalu M. Viwanja vingine ni namba 1059 kitalu Y, eneo la Mwakibete na kiwanja namba 891 kitalu M eneo la Manispaa ya Mbeya.
Mkoani Tanga eneo la New Korogwe kiwanja namba 16 kwenye kitalu B nacho umiliki wake umebatilishwa, wilayani Moshi mkoani Kilimanjaro eneo la section 111 kiwanja namba 35, kitalu HHH.
Kadhalika, mkoani Dar es Salaam, viwanja vinne vimebatilishwa miliki zake ambavyo ni viwanja viwili namba 3 kitalu F, na 278 kitalu B, vilivyoko Tegeta, na kiwanja namba 49, kitalu S na 624, kitalu N, vilivyoko Tabata.