MGOMBEA nafasi ya Naibu Spika wa Bunge kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk Tulia Ackson amesema akichaguliwa kushika wadhifa huo atafanya kazi kwa kufuata kanuni na hataegemea upande wa serikali kama inavyodhaniwa na baadhi ya watu.
Akizungumza mjini hapa jana, Dk Tulia alisema yeye ni mzoefu na waliofuatilia Bunge Maalumu la Katiba mwaka jana, waliona utendaji wake, hivyo hakuna haja ya kuwa na hofu naye.
Alisema kazi ya Naibu Spika sio kuitetea serikali wala kuibeba na kwamba jukumu la Bunge ni kuisimamia serikali, hivyo kwa Rais John Magufuli kumteua kuwa mbunge, hakuhusiani na kutaka kuegemea serikalini.
Alisema anaamini wabunge watampigia kura na atashinda nafasi hiyo na kwamba anajua changamoto zilizopo katika Bunge hilo na atakabiliana nazo ili kuhakikisha anamsaidia Spika na kulifanya liwe Bunge bora zaidi.
Dk Tulia aliyezaliwa Novemba 23, 1976 Tukuyu wilayani Rungwe mkoani Mbeya, alikuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali hadi Jumatatu wiki hii Rais Magufuli alipotengua uteuzi wake na kumteua kuwa Mbunge.
Aliteuliwa kushika wadhifa huo na Rais mstaafu Kikwete, Septemba 9, mwaka huu. Alikuwa Mjumbe wa Bunge la Katiba na ni mtaalamu katika sheria za hifadhi za jamii, kazi, uhifadhi wanyamapori, udhamini, sheria ya usimamizi wa mirathi, ufadhili miradi na madini.
Kwa upande wake, mgombea wa nafasi hiyo ya Naibu Spika kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Magdalena Sakaya ambaye ni Mbunge wa Kaliua, alisema akichaguliwa atatenda haki na atajenga heshima ya Bunge.
Sakaya, ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa CUF alisema ingawa wapinzani wapo wachache bungeni, lakini uzoefu wake ndani ya Bunge pamoja na uwezo wake, vinampa imani ya kuibuka mshindi katika uchaguzi wa leo.
Kwa mujibu wa ratiba ya Bunge, leo alasiri baada ya kumaliza jukumu la kumthibitisha Waziri Mkuu, utafanyika uchaguzi wa Naibu Spika ambapo vyama viwili ndiyo vimesimamisha wagombea.
Wakati huohuo, shughuli ya kuapishwa wabunge wa Bunge la 11 iliendelea jana, lakini kivutio kikubwa ikiwa ni ndugu, jamaa na wapambe wa baadhi ya wabunge wakiwa wamefurika nje na ndani ya viwanja vya Bunge.
Pengine kutokana na hali hiyo, baadhi ya wabunge wakati Spika akiendelea na utaratibu wa kuwaapisha wabunge kiapo cha uaminifu, wengine walikuwa hawapo ukumbini kutokana na sababu mbalimbali.
Baahi ya wabunge walikuwa nje ya viwanja vya Bunge wakijaribu kuzunguma na wafuasi wao na wengine wakihangaika kuwezesha wageni wao waingie ukumbini wakati uapishaji ukiendelea. Uapishaji wa wabunge ulioanza juzi, uliendelea jana jioni ambapo ratiba ya awali ilionesha kuwa shughuli hiyo itamalizika asubuhi.
|
0 Comments