BAADA ya kushughulikia wakwepa kodi ndani ya siku 27 alizokaa Mamlaka ya Mapato (TRA), Waziri mpya wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango amehamishia nguvu zake katika sekta ya fedha hasa benki, akizitaka zipunguze riba.
Akizungumza na waandishi wa habari Ikulu Dar es Salaam jana, baada ya kuapishwa na Rais John Magufuli, Dk Mpango aliahidi kushughulikia tatizo la riba kubwa, inayotolewa kwenye benki za hapa nchini, jambo linalochangia kushusha idadi ya watu wanaokwenda benki kukopa.

“Lazima sekta ya fedha isimamiwe vizuri ili kila mwananchi aweze kukopa, nitahakikisha riba za mikopo zinashuka ili wananchi wajipatie mikopo kwa riba nafuu,” alisema Dk Mpango.
Pia alisema atahamasisha wananchi kujiunga kwenye vyama vya ushirika, vikiwemo vya kuweka na kukopa (Vicoba). Alisema taasisi hizo zinasaidia kuwainua wananchi kiuchumi kwa kupata mikopo yenye riba nafuu na kuweka akiba zao pia.
Tatizo la riba Kwa sasa riba za mikopo katika benki mbalimbali, zimekuwa kubwa zinazofikia asilimia 21, jambo ambalo limekuwa likihojiwa na wataalamu mbalimbali, kwani mfumuko wa bei ambao ndio wenye kawaida ya kusababisha gharama za mkopo kuwa juu, upo chini ya asilimia kumi kwa muda mrefu sasa.
Aidha, kumekuwepo tofauti kubwa kati ya riba ya kuweka fedha na riba ya kukopa fedha, ambapo mwananchi akiweka fedha zake benki, amekuwa akilipwa riba ndogo ya asilimia tatu, wakati akienda kukopa fedha anatozwa riba ya asilimia mpaka 21.
Kutokana na hali hiyo, pamoja na kuwepo kwa taasisi nyingi za benki, wafanyabiashara wamekuwa wakilalamika kuwa mfumo wa fedha, umekuwa ukishindwa kukusanya akiba kwa wingi na kuiwekeza kwa wajasiriamali wa ndani ili kukuza uchumi na kuongeza ajira.
Wamachinga, viwanda Dk Mpango pia aliahidi kuwalinda wamachinga na mama lishe, ili wafanye biashara zao bila kubughudhiwa na kuongeza kipato kwa familia za kipato cha chini. “Lazima tuwaondolee kero wafanyabiashara wadogo kama mama lishe”, alisema.
Pia alisema ili Taifa lifikie katika uchumi wa kati mwaka 2025, ni lazima lijikite zaidi katika uanzishaji wa viwanda vikubwa na vidogo. Alisema hiyo ndio njia sahihi kwa taifa kujikwamua kiuchumi na kupunguza utegemezi kutoka nje ya nchi.
Ahadi hizo za kulinda wafanyabiashara ndogo ili kuongeza kipato cha familia zao na kujenga viwanda, ni miongoni mwa ahadi kubwa alizotoa Rais Magufuli, wakati alipokuwa akiomba kuchaguliwa katika nafasi hiyo na wananchi.
Katika kufanikisha ahadi hiyo ya ujenzi wa viwanda, tayari Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, amesema ni lazima kuwe na umeme wa uhakika. Katika hilo, Serikali imejipanga kuhakikisha uzalishaji wa nishati ya umeme, ambayo ndiyo kichocheo kikubwa cha uzalishaji wa viwandani, ufikie Megawati 10,000 hadi 15,000.
Ukwepaji kodi Kuhusu ukwepaji wa kodi, Dk Mpango alisema kwa kuwa hakuna Serikali inayoweza kujiendesha bila kodi, atahakikisha anaendelea kuwabana walipa kodi, kama alivyofanya ndani ya siku 27 wakati akikaimu nafasi ya Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato (TRA).
“Nawaomba Watanzania walipe kodi, kwa kweli hatutawavumilia wakwepa kodi hasa wafanyabiashara wakubwa, haiingii akilini tukimbizane na wamachinga na mama lishe halafu tuzembee kuwabana wafanyabiashara wakubwa,” alisema Dk Mpango.
Profesa Maghembe Kwa upande wake, Waziri mpya wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe ambaye uteuzi wake ulizua minong’ono huku baadhi kumpinga, alisema yeye si mzigo, kwani amefanya mambo mengi akiwa Wizara ya Maliasili na Utalii na kwenye Wizara ya Maji, alikomalizia utendaji wake wakati wa Serikali ya Awamu ya Nne.
Maji, Maliasili “Wizara ya maji ni moja ya maeneo yaliyowekwa chini ya mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) na lilikuja jopo la wataalamu kutoka nje ya nchi, kufanya tathmini ya nchi na wizara yangu ikashika nafasi ya kwanza, kati ya wizara sita zilizoko kwenye mpango huo, sasa utasemaje mimi ni mzigo?” alihoji.
Alisema alipokuwa Wizara ya Maliasili na Utalii mwaka 2007, ndio kipindi walichokamata shehena nyingi za magogo, jambo lililosaidia kulinda rasilimali za Taifa na kuongeza mapato ya nchi kwa kutumia rasilimali za nchi.
“Nasema huyo anayesema mimi ni mzigo, ni mwindaji haramu au analipwa na watu wanaowinda na mimi naomba nimtangazie kuwa kiama cha majangili kimefika, waache kazi hiyo watafute kazi nyingine ya kufanya,” alisema Profesa Maghembe wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari.
Alisema eneo la ujangili, atalisimamia kikamilifu kuhakikisha wanakomesha tatizo hilo ili kulinda uhai wa wanyama pori, ambao wanasaidia kuleta watalii nchini. Ukataji miti, watalii Pia aliahidi kulinda misitu na kupunguza tatizo la ukataji wa miti, ambalo alikiri kuwa kwa sasa unafanywa kwa kasi kubwa ili kupata nishati ya kuni.
Profesa Maghembe alisema kama kutakuwa na ulazima wa kukata kuni, iwe ni kwa mahitaji maalumu na aliahidi kutoa elimu kwa wananchi na kuongeza nishati mbadala itakayosaidia kupunguza tatizo la ufyekaji wa misitu. Kwa upande wa watalii, alisema Wizara yake itaongeza idadi ya watalii ili Taifa lipate mapato zaidi.
Alisema idadi ya sasa ya watalii ni milioni 1.2 kwa mwaka na anatarajia itaongezeka na kufikia watalii milioni 3 ili kuongeza mapato ya Taifa. Mawaziri wengine walioapishwa jana mbali na Dk Mpango, Profesa Maghembe, ni Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Gerson Lwende, Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Dk Joyce Ndalichako na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Yussuf Masauni.