WADAU kutoka Asasi za Kiraia na Kijamii katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), wamependekeza kusimamishwa uanachama kwa Burundi ili kuilazimisha serikali ya nchi hiyo, kushiriki mazungumzo ya kutafuta amani nchini humo.
Asasi hizo zimesema Serikali ya Burundi, imekuwa ikikataa kushiriki mazungumzo ya kutafuta amani nchini humo kati yake na wapinzani huku machafuko na umwagaji damu yakiendelea kutokana na mgogoro wa kisiasa.

Akiwasilisha maombi ya asasi hizo katika Kamati inayoshughulikia Usuluhishi wa Migogoro ya Bunge la Afrika Mashariki (EALA) hapa jana, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Chama cha Wanasheria wa Afrika (PALU), Donald Deya alitaka pia Burundi iwekewe vikwazo vya kiuchumi.
Deya akiwasilisha maombi hayo kwa niaba ya asasi hizo, alisema kutokana na kuongezeka kwa uvunjaji wa haki za binadamu nchini Burundi, nchi za Afrika Mashariki zinapaswa kuchukua hatua hizo, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kumaliza mgogoro huo.
“Ripoti zinaonesha kuwa hali ya uvunjaji wa haki za binadamu ikiwa ni pamoja na mauaji ni mbaya na wimbi kubwa la wakimbizi linaongezeka hivyo ni wajibu wa Bunge la Afrika Mashariki kuingilia kati ili kuepusha umwagaji wa damu,” alisema Deya na kuongeza:
Aliieleza kamati hiyo kuwa ripoti ya hali ya wakimbizi ya Tanzania ya Januari 4, mwaka huu, inaonesha kuwapo kwa wakimbizi 189,472 kutoka Burundi, kati ya hao 124,061 wakiwa wapya kutokana na kuongezeka kwa machafuko ya kisiasa nchini humo, huku mashirika mbalimbali ya kimataifa yakihamisha ofisi zao kutoka mji mkuu wa nchi hiyo, Bujumbura kutokana na kudorora kwa hali ya usalama.
“Wakuu wa nchi wanachama wa EAC wameshindwa kushughulikia suala hilo na kwa miezi sita hakuna hatua walizochukua sasa sisi kama asasi za kiraia tunaliomba Bunge lipitishe azimio la haraka la kutatua mgogoro huo kwa sababu tunaona dalili ya mauaji ya kimbari kama hatua za haraka hazitachukuliwa,” aliongeza Deya.
Pia alisisitiza kuwa wakati wa mgogoro wa kisiasa nchini Kenya, aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati Maalumu iliyoundwa, Koffi Annan alifika Kenya na wajumbe wenzake wakapata suluhisho la Kenya, sasa iweje mgogoro wa Burundi usichukuliwe hatua zinazostahili huku watu wakiendelea kufa.
Hata hivyo, baadhi ya wabunge wa EALA waliotaka ufafanuzi baada ya maombi hayo kuwasilishwa, walionesha wasiwasi wa ripoti hiyo ya asasi za kijamii kuwa imetiwa chumvi kwani mgogoro huo haujafikia hatua mbaya kiasi hicho. Mbunge Hafsa Mosi kutoka Burundi alihoji ushahidi wa tuhuma mbalimbali kuhusu hali ilivyo nchini Burundi.
Lakini, Deya katika ufafanuzi wake alikiri kutokuwa na ushahidi wa moja kwa moja zaidi ya taarifa za vyombo vya habari na ripoti ya mashirika ya haki za binadamu nchini humo. Burundi imeingia katika hali mbaya ya kisiasa baada ya kufanyika kwa uchaguzi, uliopingwa na wananchi wake na Jumuiya ya Kimataifa, ambao ulimweka madarakani Rais Pierre Nkurunziza ambaye anadaiwa kuongoza kwa muhula wa tatu kinyume cha Katiba ya nchi hiyo.