WIZARA ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeagiza kukamatwa kwa watu waliohusika kuwaozesha watoto wao wa umri wa miaka 13 na kuwakatisha masomo katika mkoa wa Shinyanga na Dodoma.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Wizara hiyo, Erasto Ching’oro alisema hayo katika taarifa yake aliyoitoa kwa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam. Ching’oro alisema wakati mtoto ambaye ni mwanafunzi wa shule ya msingi Wishiteleja wilayani Kishapu mkoa wa Shinyanga ameozeshwa kwa nguvu kwa mahari ya ng’ombe 13 na kukatishwa masomo akiwa darasa la sita, mtoto mwingine wa mtaa wa Chikole kata ya Msalato, Dodoma inasemekana ameozeshwa kwa mahari ya Sh 600,000.

Alisema kutokana na kuwepo kwa matukio hayo, Wizara ilivitaka vyombo vya dola kwa kushirikiana na Kamati za Ulinzi wa Mtoto katika mikoa yote, kuhakikisha kuwa watuhumiwa wanachukuliwa hatua kali. “Tukio la kuwaoza watoto wadogo katika umri mdogo siyo tu linakinzana na haki za msingi za mtoto bali pia linamkosesha mtoto haki ya kuendelezwa akiwa ni pamoja na kuhatarisha uhai wake kwa kupatiwa majukumu ya mtu mzima katika umri mdogo,” alisema Ching’oro.
Alisema wizara inawataka wazazi na walezi kubadilika na kuachana na tabia ya kuwaoza watoto wao katika umri mdogo, maana vitendo hivyo ni vya kikatili. Aliongeza kuwa jamii inatakiwa kutambua kuwa vitendo vya kikatili kama hivyo, vinapofanywa katika familia vinarudisha nyuma juhudi za serikali za kupambana na ukatili, maana kwa kiasi kikubwa familia inatakiwa kuwa mahala salama panapofaa watoto kuishi na kulindwa.
Pia alisema wizara inakumbusha wazazi, walezi na wadau wengine kuwa ndoa za utotoni ni kinyume cha Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009 na mikataba ya kimataifa kuhusu haki na ustawi wa mtoto.
Alisema ni wajibu wa kila mtu, kuhakikisha kuwa watoto wanaishi katika usalama na kuhakikishiwa haki zao zote za msingi, ikiwemo kulindwa, kuendelezwa, kuishi na kushirikishwa katika maisha ya kila siku ili kujenga taifa linaloheshimu maslahi ya watoto.
Juzi gazeti hili liliripoti kuwa mtoto mwenye umri wa miaka 13 anayesoma darasa la sita katika shule ya msingi Wishiteleja wilayani Kishapu, ameozeshwa kwa nguvu na wazazi wake baada ya kupokea mahari ya ng’ombe 13.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Shirika la AGAPE, John Myola, mwanafunzi huyo alifungishwa ndoa ya kimila Septemba 25, mwaka jana katika kitongoji cha Nyamikoma kijiji cha Buchambi wilayani Kishapu.
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Hawa Ngh’umbi aliyekiri kupokea nakala ya barua kutoka Agape iliyozungumzia juu ya kufungishwa ndoa kwa mtoto huyo, alikemea kitendo hicho na kuahidi kumsaka mtuhumiwa akamatwe na kufikishwa mahakamani.
Mkoani Dodoma, mama mmoja anatuhumiwa kutaka kumuozesha mtoto wake mwenye miaka 13 (jina linahifadhiwa) baada ya kupokea mahari ya Sh 600,000 na ng’ombe wanne.