WADAU wa masuala ya siasa nchini wameeleza kuridhishwa na uteuzi wa idadi kubwa ya makatibu wakuu huku wakisisitiza kwamba Rais John Magufuli apewe muda pamoja na Baraza lake la Mawaziri wafanye kazi hatimaye wapimwe kwa ufanisi wao na si kwa ukubwa au udogo wa baraza.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na gazeti hili, watu wa kada tofauti wakiwemo wasomi na wanasiasa wamesema kitendo cha Magufuli kuteua watendaji wengi ni cha kupongezwa kwani amelenga kuleta ufanisi.
Kauli hizo za kuunga mkono uteuzi wa makatibu wakuu 27 walioapishwa Januari mosi mwaka huu kuongoza wizara 19, zimekuja huku kukiwa na baadhi ya watu wanaokosoa kwa kudai Rais Magufuli hakupunguza ukubwa wa serikali bali ameongeza kutokana na kuwa na makatibu wakuu wengi.
Aliyekuwa Naibu Waziri katika Serikali ya Awamu ya Nne, Dk Makongoro Mahanga alikaririwa na baadhi ya vyombo vya habari akikosoa uteuzi huo, akidai Rais Magufuli ameunda serikali yenye wizara 27 tofauti na wizara 19 alizotangaza huku akisisitiza kuwa baraza lake la mawaziri ni kubwa.
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue akizungumza na waandishi wetu, alieleza kushangazwa na mwanasiasa huyo (ambaye sasa yuko upinzani) kutoelewa kwamba makatibu wakuu si sehemu ya Baraza la Mawaziri. “Sidhani kama kuna haja ya kumjibu.
Mtu aliyekuwa Naibu Waziri kwa muda mrefu sana, inashangaza hajui kuwa makatibu wakuu si sehemu ya Baraza la Mawaziri. Hivyo idadi yao si kipimo cha ukubwa au udogo wa baraza la mawaziri,” alisema.
Alisema, “hata wewe ukijumlisha idadi ya makatibu wakuu na naibu makatibu wakuu waliokuwepo serikali iliyopita na waliopo sasa utaona kuwa jumla yao ni wachache sasa kuliko kabla.” Kwa mujibu wa Balozi Sefue, jumla ya makatibu wakuu wa Serikali iliyopita walikuwa 54.
Rais apongezwe Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe na aliyewahi kuwa Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Joseph Kuzilwa, alisema kitendo cha Rais Magufuli kuteua watendaji wengi ni cha kupongezwa kwani amelenga kuleta ufanisi.
“Hii nchi ni kubwa na ina vitu vingi vya kusimamiwa hivyo kuteua idadi kubwa ya watendaji kwa maana ya makatibu wakuu ni sahihi kwani wao ndio wasimamizi wakuu wa sekta mbalimbali zilizo chini ya wizara husika,” alisema Profesa Kuzilwa.
Profesa Kuzilwa alisema suala si ukubwa wa baraza au serikali, bali Rais amelenga kuwa na serikali ambayo itakuwa na ufanisi mkubwa na kuleta matokeo sahihi ya utendaji. Alisema kuwa na makatibu wakuu ambao wengi wao ni wataalamu watamsaidia zaidi rais kusimamia kazi za serikali kikamilifu.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Kitivo cha Siasa na Utawala, Dk Benson Bana alisema katika fani ya utawala, haiwezekani kutumia hoja ya idadi ya makatibu wakuu kupima ukubwa au udogo wa serikali.
Dk Bala alisema pia aliyetoa hoja ya kukosoa, ambaye ni naibu waziri wa zamani, hawezi kutoa hoja iliyo katika mizani kwa kuwa ni majeruhi wa kisiasa aliyekuwa serikalini na sasa yuko kwenye upinzani.
Alisema muundo wa serikali huwa unabadilika mara kwa mara na jambo la msingi ni kuwa na watu bora wa kusaidia serikali katika kutatua matatizo ya wananchi. Acheni fitina Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labour (TLP), Augustine Mrema, aliwataka Watanzania wampe Rais Magufuli muda wa kuwatumikia kwa kuunda serikali ambayo anadhani itakuwa na tija kwa taifa.
“Naomba Watanzania tumpe Rais John Magufuli miezi sita, tuache fitina na majungu na kuanza kukosoa kosoa vitu,” alisema Mrema. Mrema alisema kuwa nchi imepata Rais mzuri na makini kwani anaongoza nchi vizuri na matokeo tumeanza kuyaona kwa kipindi kifupi kwa kudhibiti ufisadi na wizi katika maeneo mbalimbali.
Alisema Rais aachwe aunde serikali ambayo anadhani itamsaidia katika kuwaletea wananchi maendeleo na kupambana na ufisadi uliokithiri nchini, vitendo vya rushwa na hata majambazi. “Makatibu wakuu ndiyo wasimamizi wa sekali kwa ujumla,” alisema.
Mrema alisema awali walikuwa wakilalamikia ukubwa wa Baraza la Mawaziri kutokana na kukosa fedha za kulipa lakini hivi sasa matokeo yanaonesha ni mazuri kwa udhibiti wa mianya ya rushwa.
Kwa upande wake, Rais wa East Africa Bureau, Paul Mashauri, alishauri Watanzania kuwa na imani na rais na uteuzi anaoufanya kwa kuwa unalenga katika ufanisi. “Bila kujali ni baraza la namna gani, rais ameliunda lakini kubwa ambalo tunatakiwa kuliangalia ni ufanisi utakao tokana na baraza hilo pamoja na watendaji wake,” alisema Mashauri.
Awali, Dk Makongoro ambaye alihama CCM baada ya kushindwa kwenye kura za maoni, na kuingia Chadema, alikaririwa na vyombo vya habari akidai kwamba si kweli kwamba Rais Magufuli amepunguza ukubwa wa serikali bali ameongeza.
“Sina hakika kama wasaidizi wa rais wamemshauri na kumweleza kwamba wizara si ofisi ya waziri bali wizara ni ofisi ya Katibu Mkuu (mtendaji mkuu, afisa masuhuli). Mtendaji mkuu ndiye mwenye dhamana.
Ndiyo maana hata katika ngazi ya kata, ofisi ile inaitwa Ofisi ya Ofisa Mtendaji wa kata siyo ofisi ya Diwani,” Mahanga alinukuliwa. Alidai kwamba, ukubwa wa serikali hautegemei sana wingi wa mawaziri bali wingi wa makatibu wakuu huku akisema ahadi ya Rais Magufuli kwenye kampeni kwamba ataunda serikali ndogo hakuitimiza.
|
0 Comments