NAIBU Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yussuf Masauni ameliagiza Jeshi la Polisi kuwasimamisha kazi askari watatu wa Kikosi cha Zimamoto cha Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam kutokana na tuhuma za wizi wa mafuta ya ndege pamoja na mizigo ya abiria.
Alitaja majina ya askari hao kuwa ni Abias Mwanza, Khalfani Kisana na Musa Mandauli ambao wote wanatoka Kikosi cha Zimamoto katika JNIA. Aidha, Naibu Waziri ameiagiza Idara ya Uhamiaji kwenye uwanja huo wa ndege kufanya uhakiki wa mapato yanayotokana na viza zinazotolewa kwa wageni kwani imebainika kuwa idadi ya viza zinazotolewa kwa wageni hailingani na mapato yanayopatikana.

Masauni alitoa maagizo hayo jijini Dar es Salaam jana, alipofanya ziara kwenye vitengo mbalimbali vya kiwanja hicho, ikiwa ni sehemu ya ukaguzi wa taasisi zote ambazo ziko chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, ikiwamo Jeshi la Polisi na Idara ya Uhamiaji.
Katika ziara hiyo ambayo ilianzia Makao Makuu ya Jeshi la Polisi na kwenda JNIA kisha Kituo cha Polisi cha Buguruni katika Wilaya ya Ilala, Naibu Waziri Masauni alikiri kwamba licha ya kazi nzuri inayofanywa na Jeshi la Polisi, lakini bado uaminifu kazini bado ni changamoto kwa baadhi ya askari.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri, Agosti 26, mwaka jana askari Kisana na Mandauli wanatuhumiwa kukamatwa na dumu 10 za ujazo wa lita 20 zikiwa zimejaa mafuta ya ndege zikisafirishwa kutoka kiwanjani hapo kwa kutumia gari aina ya Land Rover lenye namba za usajili STJ 2948 ambalo ni la Mkuu wa Kikosi cha Zimamoto JNIA.
Mtuhumiwa Mwanza ambaye pia ni askari anatuhumiwa kushirikiana na mfanyakazi wa Kampuni ya Swissport, Lucas Maganda baada ya kunaswa na kamera za kiwanjani hapo wakishirikiana kutoa mizigo ya abiria kinyume cha utaratibu kutoka kwenye eneo la kuhifadhia mizigo.
“Naagiza askari hawa wasimamishwe kazi mara moja ili kupisha uchunguzi dhidi ya tuhuma zinazowakabili,” alisema Naibu Waziri na kuongeza kuwa wakibaini kama makosa wachukuliwe hatua kali za kisheria.