Spika wa Bunge, Job Ndugai.
WABUNGE na wanasiasa wametaka Bunge lichunguzwe kutokana na tuhuma kwamba baadhi ya wabunge wakiwamo wenyeviti wa baadhi ya Kamati za Kudumu za Bunge, wanahusishwa na upokeaji wa rushwa. Juzi Spika wa Bunge, Job Ndugai alitangaza kufanya mabadiliko ya wajumbe 27 wa Kamati za Kudumu za Bunge yaliyowang’oa wenyeviti watano.
Hata hivyo, Ofisi ya Bunge imesisisiza kuwa mabadiliko hayo, hayajatokana na tuhuma za rushwa kwa baadhi ya kamati hizo kama inavyozushwa. Badala yake imesema ni ya kawaida na kwamba katika mabadiliko, Spika hakuainisha dosari zozote katika utendaji wa kamati hizo za Kudumu za Bunge.

Hata hivyo, licha ya kauli hiyo, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maendeleo na Huduma za Jamii jana ilishindwa kufanya vikao vyake baada ya wajumbe wengi kuingia mtini, kwa madai wanataka Spika atoe muongozo kuhusu kujiuzulu kwa wenzao wawili waliofanya hivyo kutokana na uwepo wa tuhuma za rushwa zinazoigusa kamati hiyo.
Kutokana na hilo, wabunge wametaka kufanyike uchunguzi ili kama kuna wabunge waliokula rushwa wajulikane na kama hakuna, basi chombo cha habari kilichoandika kuhusu madai hayo kichukuliwe hatua. Ratiba ya jana ya kamati hiyo inayokutana Dar es Salaam ilikuwa ikutane na wizara tatu za Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Watoto na Wazee, Elimu, Teknolojia na Ufundi na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).
Kukutana kwa wizara hizo, kulitokana na maagizo ya awali yaliyotolewa wiki iliyopita kwenye kamati hiyo na aliyekuwa Mwenyekiti wake, Dk Raphael Chegeni kwamba wizara hizo tatu zikutane na kamati kwa pamoja ili kila mmoja aeleze majukumu na mipaka yake kwa lengo la kuondoa utata uliopo baina yao.
Hata hivyo, hiyo jana baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo wakiwemo Dk Ely Macha, Susan Lyimo, Juma Nkamia, Kasuku Bilago na Lucy Mlowe walifika kwenye ukumbi wa kikao hicho cha kamati na kuwakuta baadhi ya watumishi wa Bunge wa kamati hiyo ila kikao hakikuwepo.
Lyimo alisema kikao hakijafanyika kwa sababu ya baadhi ya wenzao kujiuzulu akiwemo Mbunge wa Kigoma Mjini, Kabwe Zitto aliyemuandikia Spika barua ya kujiuzulu kwake nafasi ya ujumbe ndani ya kamati hiyo ili kupisha uchunguzi wa madai ya rushwa ndani ya kamati hiyo.
Aidha, Mjumbe mwingine aliyejiuzulu nafasi yake ni Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe. Akizungumzia hali hiyo, Lyimo alisema yeye na baadhi ya wenzake walifika jana asubuhi kwenye ukumbi wa kikao ila hakikufanyika na maelezo waliyopewa ni kutokana na kujiuzulu kwa wenzao na hivyo wanasubiri amuongozo wa Spika. “Ni kweli tumekuja kwenye kikao kama ratiba ilivyokuwa ila tumeona wenzetu wengi hawapo, tumekuja wachache na hakuna kinachoendelea, tumeondoka hadi kesho(leo),” alisema Lyimo.
Kwa upande wake, Bilago alisema ni kweli hawajakutana kutokana na mambo mbalimbali yakiwemo tuhuma za rushwa zilizofanya baadhi ya wajumbe kujiuzulu na wao wameomba uchunguzi ufanyike ili kubaini ukweli wake. “Tumeomba uchunguzi ufanyike kama kweli wapo wajumbe waliokula rushwa hatua zichukuliwe na kama madai hayo sio ya kweli, basi mwandishi na vyombo husika vya habari vilivyoripoti tuhuma hizo vichukuliwe hatua,” alisema Bilago.
Alisema pamoja na baadhi yao ndani ya kamati kujiuzulu kupisha uchunguzi dhidi ya tuhuma hizo, wao hawajajiuzulu ndio maana wameendelea kuhudhuria vikao vya kamati hiyo na kwamba wanachokitaka wao ni uchunguzi ufanyike ili ukweli uwekwe bayana.
Hoja ya wabunge hao iliungwa mkono na chama cha siasa cha ACT Wazalendo ambacho kilimtaka Spika Ndugai kuitisha mara moja uchunguzi kwa kamati zote zilizotuhumiwa ili ukweli ubainike na hatua za kisheria zichukuliwe mara moja, kwani kuwahamisha kamati wabunge kamwe hakutaondoa tatizo na kulirejeshea Bunge hadhi yake.
Akizungumza jana na waandishi wa habari Dar es Salaam, Mwenyekiti, Kamati ya Bunge na Serikali za Mitaa wa ACT Wazalendo, Yeremia Maganja alisema ACT wamesikitishwa na uamuzi huo wa Spika kuwahamisha kamati Wenyeviti, Makamu Wenyeviti na wajumbe wa baadhi ya Kamati za Kudumu za Bunge uliofanywa juzi. Maganza alisema kimsingi utamaduni huo unafifisha mapambano dhidi ya rushwa na uwajibikaji kwa viongozi wa umma na watendaji wa serikali.
Lakini taarifa ya Ofisi ya Bunge iliyotolewa jana na Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano cha Bunge kwa vyombo vya habari ilisema msingi wa mabadiliko hayo umelenga kuzingatia mahitaji mapya na changamoto zilizojitokeza baada ya kuundwa kwa kamati hizo Januari mwaka huu na kwamba Spika alikuwa ameanza kufanyia kazi mabadiliko hayo tangu mapema mwezi huu.
“Waheshimiwa wabunge wanaosakamwa kwa uvunjifu wa maadili kupitia mitandao ya kijamii na magazeti, ni budi wakatendewa haki kwa sababu Spika anazingatia sana utawala wa sheria. “Kama kuna mbunge yeyote anayetuhumiwa kwa makosa ya jinai, mamlaka za kiuchunguzi zina wajibu wa kutekeleza majukumu yao na pale inapobidi Bunge lenyewe kupitia Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge inaweza kufanya uchunguzi kwa Mamlaka ya Spika,” ilisema taarifa hiyo.
Awali, asubuhi akizungumza na kipindi cha Power Breakfast kinachorushwa na redio ya Clouds FM Dar es Salaam, Spika Ndugai alisema mpaka sasa hakuna mbunge yeyote anayechunguzwa kwa tuhuma za rushwa na Bunge hilo, ingawa kuna uwezekano vyombo vya dola vikawa vinaendesha uchunguzi kwa baadhi ya wabunge.
“Hakuna taarifa yoyote ya rushwa dhidi ya wabunge niliyonayo, hizo taarifa za rushwa nimezisikia huko kwenye vyombo vya habari na hazihusiani na mabadiliko haya ya wajumbe wa kamati,” alisisitiza Ndugai. Imeandikwa na Halima Mlacha, Mroki Mroki na Oscar Mbuza.