RAIS John Magufuli amemwapisha Mkuu wa Mkoa mpya wa Songwe, Luteni mstaafu Chiku Gallawa, ambaye hakuapishwa pamoja na wakuu wa mikoa wenzake Machi 15, mwaka huu.
Sherehe ya kumwapisha ilifanyika Ikulu jijini Dar es Salaam jana na kuhudhuriwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa. Luteni mstaafu Gallawa anakuwa Mkuu wa Mkoa wa kwanza kwa Mkoa mpya wa Songwe, ulioanzishwa kwa kuugawa mkoa wa Mbeya, uliopo Kusini mwa Tanzania.

Wakati huo huo, Rais John Magufuli amepokea taarifa ya ukaguzi wa hesabu za serikali kutoka kwa Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad, Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais Magufuli amepokea taarifa hiyo yenye ripoti tano, ikiwa ni utaratibu wa kikatiba unaomtaka CAG kukabidhi kwa Rais taarifa ya ukaguzi kabla ya mwisho wa mwezi Machi.
Baada ya kupokea taarifa hiyo, Rais Magufuli ataikabidhi mbele ya Bunge katika siku saba za mwanzo za kikao kijacho cha Bunge, kitakachofanyika mjini Dodoma. Rais Magufuli alimpongeza Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali na timu yake kwa kuandaa taarifa hiyo.
Alitoa mwito kwa chombo hicho, kuendelea kufanya kazi kwa uhuru na ufanisi, huku akiahidi kuwa serikali itatoa ushirikiano wa kutosha kufanikisha kazi zake.