WIZARA ya Nishati na Madini imewahakikishia Watanzania kuwa Tanzania ina uhakika wa asilimia 98 za kupata mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Uganda kwenda bandari ya Tanga, ambao unapiganiwa pia na nchi jirani ya Kenya.
Kutokana na hali hiyo, wizara hiyo jana imefanya mkutano na wafanyabiashara wa sekta ya mafuta, kuwaeleza fursa zilizopo kwenye mradi huo, jambo ambalo limewasukuma wafanyabiashara hao kuazimia leo kwenda Uganda kukutana na Serikali ya Uganda, kuwaeleza faida itakazopata nchi hiyo kwa kuleta mradi huo nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Justin Ntalikwa, alikiri kuwa bado upo mvutano mkubwa wa wapi mradi huo ujengwe kutokana na Kenya kupambana kuhakikisha inapata mradi huo. Alisema hadi juzi walikuwa wanaendelea kufanya mazungumzo kati ya Uganda na Kenya.
Hata hivyo, alisema Tanzania ipo kwenye nafasi nzuri zaidi ya kushinda vita hiyo kutokana na vivutio vilivyopo, ikiwa ni pamoja na gharama ndogo za ujenzi wa bomba hilo ikilinganishwa na ujenzi wa kwenda Kenya. “Nasema hivyo kwa sababu sisi tunazo sifa nyingi ambazo Uganda inashawishika kuuleta mradi huo hapa kwetu ikiwa ni pamoja na usalama uliopo nchini kuliko Kenya, uzoefu wa kujenga mabomba ya namna hiyo kwani hadi sasa tunayo mabomba manne ya namna hiyo,” alisema Profesa Ntalikwa.
Alitaja sifa nyingine kuwa ni kina kirefu cha bandari ya Tanga, ukilinganisha na bandari za Lamu na Mombasa. “Ndiyo maana nasema tuna fursa ya asilimia 98 ya kupata mradi huu kuliko wenzetu na Uganda wameridhika na vivutio vya kwetu,” alisema.
Alisema kutokana na uhakika wa kupata mradi huo, ndiyo maana wameamua kufanya mkutano na wawekezaji wa sekta ya mafuta nchini waone fursa zilizopo kwenye mradi huo na zabuni ambazo wanaweza kuomba na ajira zinazopatikana katika mradi wenyewe na aina ya kodi itakayolipwa wakati wa mradi.
Kauli ya wafanyabiashara Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyabiashara, Dk Gidion Kaunda alisema mkutano wa jana umehusisha wafanyabiashara wapatao 40 na wote kwa pamoja wameazimia leo kwenda Uganda kuzungumza na Rais Yoweri Museveni kuhakikisha kwamba mradi huo wa bomba unaletwa nchini. “Huu ni ushindani wa kibiashara, sisi tuko tayari kushirikiana na Serikali kuhakikisha tunaupata mradi huu wa bomba, hii ni fursa nzuri kwa nchi yetu.
Tumeamua kujitoa mhanga kesho (leo) tunaenda kuzungumza na Serikali ya Uganda,” alisema. Alisema wanaenda kuieleza Serikali ya Uganda sifa za Tanzania miongoni mwake ikiwa ni uzoefu wa kujenga mabomba hayo, usalama pamoja ujuzi wa teknolojia kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC).
Dk Kahunda alisema umefika wakati Watanzania kuwa na kasi ya kuchangamkia fursa za kibiashara zilizopo kama huo wa ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Uganda kwenda bandari ya Tanga. Alitoa mwito kwa vyombo vya habari kuisaidia Serikali kupigia debe mradi huo ambao unanyemelewa kwa nguvu na Serikali ya Kenya.
“Wenzetu wa Kenya wanajua thamani ya mradi huu, wanaangalia miaka 15 ijayo ndio maana wanafanya kila linalowezekana kuhakikisha bomba hilo linajengwa kwenda Mombasa,” alisema Dk Kaunda. Mvutano na Kenya Akizungumzia hatua ya Kenya ya kutaka kupora mradi huo, Profesa Ntalikwa alisema Serikali ya Tanzania inaendelea na mazungumzo na Serikali za Uganda na Kenya kuhusu ujenzi wa mradi huo wa bomba la mafuta.
Alipoulizwa inakuwaje Tanzania ifanye mazungumzo na Kenya wakati mradi ni wa Uganda, Katibu Mkuu huyo alifafanua kuwa Serikali ya Kenya ndio waratibu wa mradi huo katika ukusanyaji wa taarifa za awali kuhusu ujenzi wa bomba la mafuta na uamuzi utakaofikiwa. Alisema ipo kamati iliundwa na ilihusisha maofisa wa Uganda na Kenya wakati wanaanza mchakato wa kukusanya taarifa za awali kuhusu ujenzi wa bomba hilo.
“Sisi Tanzania hatukuhusishwa katika hatua za awali na hivyo hatukuwemo kwenye kamati hiyo inayokusanya taarifa za awali za ujenzi wa mradi huo,” alisema. Alisema kamati hiyo ya wataalamu kutoka nchi hizo mbili ndio iliyoamua kukusanya takwimu hizo kuanzia Lamu, Mombasa na Tanga jambo ambalo wamelifanya na kubaini kuwa Tanga ndio sehemu yenye sifa zote za kujengwa kwa bomba hilo japo Kenya haitaki kukubaliana na matokeo ya utafiti huo.
“Na hata tulipokuja kuhusishwa sisi tumeshatoa msimamo wetu kuwa hatutashiriki katika ukusanyaji wa taarifa kwenye bandari za Lamu na Mombasa; badala yake tutashiriki tu katika taarifa zinazohusu bandari ya Tanga,” alisema Profesa Ntalikwa.
Akizungumzia mbinu zinazofanywa na Kenya ikiwa ni pamoja na kuleta wajumbe kukagua bandari ya Tanga wakati ujumbe uliokaribishwa ilikuwa ni kutoka Uganda peke yake, alisema kwamba Tanzania iliwazuia mawaziri kutoka Kenya kuingia bandari ya Tanga kwa kuwa hawakualikwa.
“Ni kweli walikuja maafisa kutoka Kenya, lakini tuliwazuia wasiende Tanga, waliishia uwanja wa ndege. Ila wale Waganda ambao tuliwakaribisha tuliwaruhusu kwenda bandari ya Tanga kukagua na kuchukua taarifa walizotaka,” alifafanua na kuongeza kuwa kwa kuwa suala hilo ni la kidiplomasia na Tanzania itaendelea kuchukua hatua stahiki .
Aliongeza kuwa Tanzania imejipanga na inaendelea kufuatilia kwa karibu ili mradi huo usichukuliwe na Kenya wakati sifa zinazotakiwa ziko Tanzania. Alisema makubaliano ya ujenzi wa bomba hilo yakikamilika ikiwa ni pamoja na njia litakakopita ujenzi wake utachukua miezi 36 pekee.
Kuhusu mradi wenyewe Ujenzi wa bomba hilo utagharimu dola za Marekani bilioni nne na litakuwa na urefu wa kilometa 1,410. Ujenzi wake ukianza Agosti mwaka huu utamalizika mwaka 2020 na utatoa ajira kwa watu zaidi ya 1,500.
Kenya ina nafasi ya kupoteza mradi huo kwa kuwa gharama za ujenzi ni kubwa kwani zinafikia dola za Marekani bilioni 4.5. Kulingana na taarifa ya TPDC, ujenzi wa mradi huo utaanzia katika Bonde la Ziwa Albert ambako ndiko mafuta ya Uganda yatachimbwa na mtambo wa mradi utajengwa katika eneo la Hoima ambako bomba litaanzia na kupitia maeneo ya Kaskazini Magharibi mwa Tanzania kwenye mikoa ya Kagera na Singida hadi bandari ya Tanga.
TPDC imewahakikishia wanaharakati ambao nao wameingia kwenye mkumbo wa kupinga ujenzi wa bomba hilo kuwa hautapitia katika hifadhi ya taifa ya wanyama na pia ujenzi wake utakwepa milima pamoja na makazi ya watu.