|
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, imemnyima dhamana aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Harry Kitilya na wenzake wanaokabiliwa na mashitaka ya utakatishaji wa fedha.
Hakimu Mkazi Mkuu, Emilius Mchauru aliwanyima dhamana washitakiwa hao kwa kuwa mashitaka yanayowakabili hayana dhamana kisheria.
Akisoma uamuzi wa ombi la dhamana lililokuwa limewasilishwa na washitakiwa hao kupitia kwa mawakili wao, Hakimu Mchauru alisema mashitaka hayo hayana dhamana kisheria, pia kwa mujibu wa uamuzi uliotolewa katika Mahakama Kuu, makosa ya utakatishaji wa fedha yanaathiri uchumi, hivyo hayapaswi kutolewa dhamana.
Awali kabla ya kutolewa kwa uamuzi huo, mawakili wa washitakiwa hao wakiongozwa na Wakili Alex Mgongolwa, waliiomba Mahakama waondoe ombi hilo la dhamana walilokuwa wamewasilisha, lakini mahakama ilikataa na kutoa uamuzi huo kwa sababu kwa kufanya hivyo wangezuia mahakama isifanye kazi yake.
Baada ya kutolewa kwa uamuzi, Wakili Mgongolwa aliiomba mahakama iwafutie washitakiwa shitaka la utakatishaji wa fedha kwa kuwa hati ya mashitaka haina maelezo yanayokidhi vigezo vya kisheria vya shitaka hilo, jambo ambalo lilizua mabishano ya kisheria.
Mgongolwa alidai ili shitaka liweze kuwa la utakatishaji wa fedha ni lazima kuwe na hatua nne; kwanza kuwe na kuwekwa kwa fedha, kuhamishwa kwa fedha na fedha kuwekwa kwenye shughuli za kiuchumi kwa lengo la kuficha, pia kuwe na chanzo kichafu cha fedha.
Alidai katika maelezo ya mashitaka, upande wa Jamuhuri haujaeleza hatua zote bali wametumia kifungu cha 12 (a) cha Sheria ya Kuzuia Utakatishaji wa Fedha, ambacho kinagusia kuhamisha fedha tu badala ya kutumia kifungu cha 12 a, b,c na d.
Hata hivyo, upande wa Jamuhuri ukiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Osward Tibabyekoma, ulipinga na kuomba mahakama itupilie mbali ombi hilo kwa kuwa halina msingi kisheria na pia hati hiyo imekidhi maelezo yote ya kosa la utakatishaji wa fedha.
Alifanunua kuwa, kosa hilo lina hatua tatu ambazo ni kuweka fedha, kuhamisha na kuziweka kwenye shughuli za uchumi. Wakili Mgongolwa alipinga na kudai, Wakili Tibabyekoma anapotosha na kuiomba mahakama ikubali ombi lao na kufuta shitaka hilo.
Baada ya mabishano ya muda mrefu Hakimu Mchauru aliahirisha kesi hiyo hadi Aprili 22, mwaka huu atakapotoa uamuzi.
Washitakiwa walirudishwa rumande. Mbali na Kitilya washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni mrembo wa zamani wa Tanzania ambaye pia alikuwa Mkuu wa Uwekezaji wa Benki ya Stanbic, Shose Sinare na aliyekuwa Mkuu wa Kitengo cha Sheria wa benki hiyo, Sioi Graham Solomon.
Mashitaka mengine yanayowakabili katika kesi hiyo mbali na kutakatisha fedha, ni pamoja kutumia nyaraka za kughushi na za uongo kujipatia isivyo halali Dola za Marekani milioni sita, sawa na Sh bilioni 12 za Tanzania.
Wanadaiwa katika tarehe tofauti kati ya Agosti 2012 na Machi 2013, jijini Dar es Salaam, washitakiwa hao watatu walipanga pamoja kwa kushirikiana na watu wengine ambao hawakufikishwa mahakamani hapo, kutenda kosa la kujipatia fedha kwa udanganyifu kutoka serikalini.
Ilidaiwa kuwa kati ya Agosti 2, 2012 katika Makao Makuu ya Benki ya Stanbic Tanzania Limited yaliyopo wilayani Kinondoni, Sinare akiwa na nia ovu, alighushi taarifa ya maombi ya fedha ya Benki ya Standard ikiwa na tarehe ya Agosti 2, 2012.
Kwa mujibu wa madai hayo, Sinare alieleza katika maombi hayo kuwa Benki ya Standard ya London kwa kushirikiana na Benki ya Stanbic ya Tanzania, watatoa mkopo unaofikia Dola za Marekani milioni 550 kwa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa gharama ya asilimia 2.4 ya mkopo huo, wakati akijua kuwa gharama hiyo si kweli.
Inadaiwa kuwa, Agosti 13, 2012, mrembo huyo wa zamani wa Tanzania, aliwasilisha taarifa hiyo ya kughushi katika Wizara ya Fedha iliyopo Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam. Kwa mujibu wa madai hayo, Septemba 20, 2012 katika Benki ya Stanbic, Sinare alitengeneza na kuwasilisha barua ya uongo ya kuelezea mkopo huo wa Dola za Marekani milioni 550, ikieleza kuwa Benki ya Standard PLC kwa kushirikiana na Benki ya Stanbic, zitatoa mkopo huo kwa Serikali kama wakikubaliwa.
Katika mashitaka mengine inadaiwa, Novemba 5, 2012 katika Benki ya Stanbic jijini Dar es Salaam, washitakiwa wote watatu, wakiwa na nia ovu, walitengeneza makubaliano ya uongo kwa lengo la kuonesha kuwa benki imeipa kampuni ya Enterprise Growth Market Advisors (EGMA) Limited, kazi ya kushughulikia mkopo huo.
Lengo la washitakiwa hao kwa mujibu wa madai hayo, lilikuwa kufanikisha mkopo huo wa Dola za Marekani milioni 550 kwa Serikali ya Tanzania, ambapo EGMA alitarajiwa kuonekana kuwa muongozaji wa mazungumzo ya kupata mkopo huo.
Ilidaiwa kuwa Machi 2013 jijini Dar es Salaam, Kitilya, Sinare na Sioi, wakiwa na lengo ovu walifanikiwa kupata Dola za Marekani milioni sita, sawa na Sh bilioni 12, wakidai kuwa fedha hizo ni malipo ya kazi iliyofanywa na EGMA Limited.
Katika shitaka la utakatishaji fedha wanadaiwa kati ya Machi 13 na Septemba mwaka jana, kwa pamoja walitakatisha Dola za Marekani milioni sita kwa kuzihamisha kwenda katika akaunti tofauti, kuzitoa katika akauti hizo na kuziweka katika akauti nyingine tofauti zinazomilikiwa na EGMA Limited katika Benki ya Stanbic Tanzania Limited na Benki ya KCB Limited.
0 Comments