CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimemjibu aliyekuwa mgombea urais kupitia Chadema, Edward Lowassa, kuwa Rais John Magufuli hafanyi kazi kwa kutafuta umaarufu, bali kwa kutekeleza alichowaahidi Watanzania.
Hatua hiyo imekuja baada ya Lowassa kukutana na kufanya mazungumzo na wanazuoni kutoka katika vyuo vikuu mbalimbali vya ndani na nje ya nchi ambapo aligusia masuala mbalimbali ikiwemo hali ya kisiasa nchini na kutimuliwa kwa watumishi wenye tuhuma na tatizo la mfumo nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari jana katika Ofisi Ndogo za Makao Makuu ya chama hicho yaliyopo Mtaa wa Lumumba, Msemaji wa chama hicho Christopher Ole Sendeka alisema, alichokifanya Lowassa ni kutaka kuwaaminisha Watanzania kuwa masuala anayoyafanya Rais Magufuli ni ya kisiasa, jambo ambalo si kweli.
Alisema ili aweze kushughulika na matatizo ya wananchi ni lazima serikali izibe mianya yote ya rushwa, upotevu wa fedha za serikali ili iweze kukusanya nguvu za serikali kushughulikia ustawi wa watu na kuleta maendeleo ya wananchi, kazi iliyofanywa kwa ufasaha mkubwa na Rais Magufuli.
Alisema katika kufanya hayo ni lazima awaguse watu kwa sababu mianya ya ubadhirifu na upotevu wa fedha za serikali unafanywa na watumishi wasio waamini na kwamba serikali ya Magufuli haijawahi kumfukuza mtu bila kumpa haki ya kusikilizwa na hata waliosimamishwa wakati wakisubiri kupata fursa ya kujitetea na serikali kujiridhisha juu ya tuhuma zao.
Alisema kitendo cha Lowassa kusema anasononeshwa na watumishi kufukuzwa kazi bila kufuata taratibu, si jambo la kweli bali analenga kujitafutia umaarufu.
Akifafanua kuhusu suala la kimfumo, Sendeka alisema Tanzania haina tatizo kubwa la kimfumo kwani mifumo imekuwa ikirekebishwa mara kwa mara katika awamu zote na mfumo wa uongozi wa uendeshaji serikali haujawa na athari ya kuwa chanzo cha uzembe au kuwa kichaka cha watuhumiwa wa ufisadi.
Alisema pamoja na Lowassa kulalamikia kuwa mfumo ni mbovu, alipokuwa Waziri Mkuu hakuna hatua madhubuti alizochukua katika tatizo la mfumo na hakuweka bayana, ni tatizo lipi au mfumo gani unaohitaji marekebisho.
Alisema hatua zinazochukuliwa na serikali zinatokana na matumizi mabaya ya madaraka yaliyokuwa yakifanywa na baadhi ya watumishi, ikiwemo ubadhirifu, uhujumu uchumi na ukwepaji wa kodi uliokithiri.
Aliongeza kuwa katika kupambana na ufisadi haitakiwi kuangalia mtuhumiwa anatoka katika chama kipi, bali hata kama ni CCM au Chadema lakini ni fisadi ni lazima achukuliwe hatua.
|
0 Comments