Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Phillip Mpango
BUNGE la Bajeti linaanza mkutano wake leo mjini hapa, huku Ofisi ya Waziri Mkuu ikiwa ya kwanza kuwasilisha hotuba yake ya makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2016/17 itakayojadiliwa kwa siku tatu.
Kadhalika, katika Bunge hilo mahususi kwa ajili ya kujadili na kupitisha Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2016/17, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Phillip Mpango anatarajiwa kuwasilisha hotuba ya Bajeti ya Serikali Juni 9, mwaka huu na kisha wabunge kuijadili kwa siku tisa.

Mkutano huo wa Bunge pia utatoa nafasi kwa serikali kujibu jumla ya maswali 465 yatakayoulizwa na wabunge mbalimbali huku maswali 88 ya Papo kwa Hapo kwa Waziri Mkuu yakitarajiwa kuulizwa kila Alhamisi.
Katika Bunge hilo litakalokaa kwa takribani siku 73, wizara zote 18 zitajadili hotuba zao ndani ya siku 47 na kufuatiwa na mjadala wa Bajeti ya Serikali utakaojadiliwa na kuhitimishwa kwa wabunge kupiga kura ya wazi kwa mujibu wa Kanuni ya 107 ya Kanuni za Kudumu za Bunge za mwaka 2013.
Kwa mujibu wa taarifa na ratiba ya mkutano huo wa Bunge la Bajeti iliyotolewa jana mjini hapa, Ofisi ya Waziri Mkuu itakuwa wizara ya kwanza kuwasilisha bajeti yake.
Wizara hiyo inayoshughulika na masuala nyeti ya kijamii kama vile vijana, kazi na ajira, inatarajiwa kuwasilisha bajeti itakayoonesha mpango wa kuboresha programu za kukuza fursa mbalimbali za makundi yaliyo kwenye wizara hiyo.
Kikubwa zaidi kinachotarajiwa kuonekana katika bajeti hiyo ni jinsi ilivyojipanga kutekeleza programu za kukuza fursa za ajira kwa makundi ya vijana,walemavu na pia maeneo ya kazi kwa kuhakikisha waajiriwa wanakuwa na mikataba ya ajira yenye maslahi.
Wakati wizara hiyo ikijadili bajeti hiyo kwa siku tatu kuanzia Ijumaa wiki hii, wizara itakayofuata kujadili bajeti yake ni Ofisi ya Rais ambayo inashughulikia Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) itakayojadiliwa kwa siku tatu kisha kufuatiwa na Utumishi na Utawala Bora itakayojadiliwa kwa siku moja.
Wizara ya tatu itakayowasilisha bajeti yake ni Ofisi ya Makamu wa Rais inayoshughulikia Muungano na Mazingira, itakayojadiliwa kwa siku moja ambayo ni Mei 3, mwaka huu ambapo mambo kadhaa wa kadha yanayohusu mazingira na Muungano yakitegemewa kuwasilishwa.
Wizara nyingine kwa mtiririko wa kuwasilisha makadirio yao ni Kilimo, Mifugo na Uvuvi itakayojadiliwa kwa siku mbili, Katiba na Sheria itafuatia kuwasilisha bajeti yake itakayojadiliwa kwa siku moja, Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa itakayojadili bajeti yake kwa siku moja ikifuatiwa na Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa siku mbili. Baada ya hizo ni Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto itakayojadiliwa Mei 12 na kufuatiwa na Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo itakayojadiliwa kwa siku moja na Mambo ya Ndani ya Nchi pia kwa siku moja.
Pia Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa pamoja na Fedha na Mipango zitawasilisha bajeti zao kila moja kwa siku moja, wakati Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Nishati na Madini, Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Maliasili na Utalii, Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi pamoja na Maji na Umwagiliaji zitawasilisha kila moja bajeti yake kwa siku mbili.