Hali ya Usalama katika Kituo cha Afya
cha Kata ya Buzuruga kilichopo Manispaa ya Ilemela Mkoani Mwanza imeimarika,
baada ya Wakazi wa Kata hiyo wanaounda Kikundi cha Kijamii cha “Ulipo Tupo”
kufyeka vichaka vilivyokuwa katika kituo hicho ambavyo vilikuwa vikitumiwa na
wahalifu kama maficho yao.


Baada ya kufyeka vichaka hivyo jumamosi iliyopita, Mwenyekiti wa Kikundi hicho, Ndaisaba
Aron alisema kuwa vichaka hivyo vilikuwa hatarishi kwa wananchi, wagonjwa
pamoja na wahudumu wa Afya katika Kituo hicho, kutokana na kupata malalamiko
kwamba vibaka walikuwa wakikimbilia katika vichaka hivyo baada ya kufanya
uhalifu.

Hidaya
Bashiru ambae ni mwanachama wa kikundi hicho pamoja na Sixtus Ijugo ambae ni
Katibu, waliwasihi wananchi wengine kuwa na desturi ya kushiriki katika
shughuli za kijamii ikiwemo katika maeneo mbalimbali kama hospitali, shule na
kwingineko kwa ajili ya maendeleo yao wenyewe.

Diwani
wa Kata ya Buzuruga, Richard Machemba, alijumuika na Kikundi hicho kwa ajili ya
kufanya usafi katika Kituo hicho ambapo alipongeza juhudi mbalimbali
zinazofanywa na wakazi pamoja na vikundi mbalimbali vya maendeleo katika Kata
yake ambapo amewasihi wananchi kuendelea kujitoa kwa ajili ya kushiriki
shughuli za maendeleo.
Sikiliza Sauti HAPA