KATI ya wanawake wa Kitanzania waliopeperusha bendera yetu vizuri nje ya nchi kielimu ni Kapteni Hilda Wendy Ringo ambaye sasa ni rubani.
Elimu yake ya sekondari aliipata katika Shule ya Tambaza jijini Dar es Salaam na baadaye Chuo Cha Urubani cha Progress Flight Academy cha jijini Pretoria, Afrika Kusini.
Ni mwanamke wa kujivunia katika nchi yetu kwa sababu amekuwa akirusha ndege yaani rubani. Amewahi kuhojiwa na vyombo mbalimbali vya habari nchini na kuhusu kazi yake hiyo anasema: “Kurusha ndege ni jambo zuri linalofurahisha.”
Rubani Hilda ni mama mwenye umri wa miaka 33, anasema alianza kurusha ndege akiwa na umri wa miaka 22 lakini sasa anarusha ndege hapahapa nchini katika Kampuni ya Precision Air. Ana uzoefu mkubwa na kazi hiyo ya urubani kwa sababu ameifanya kwa zaidi ya miaka 10 sasa na ni mwanamke wa kwanza Mtanzania kurusha ndege aina ya Boeing Airbus.
Anasema wazo la kuwa rubani lilimuingia katika akili yake akiwa bado mdogo baada ya kujiuliza maswali mengi kama vile ndege ambayo ni chuma na mabati inawezaje kupaa angani? Anasema swali hilo lilimjia wakati anasafiri mara kwa mara na wazazi wake akitokea Kilimanjaro kuja Dar es Salaam akitumia Shirika la Ndege la Tanzania (Air Tanzania) lilipokuwa linatamba katika anga ya Tanzania enzi hizo. Kapteni Hilda akizungumzia wanawake wenzake anasema: “Tanzania ina hazina kubwa ya wanawake si tu kupitia kwenye elimu nzuri, mtu anayoweza kuitumia kuwa ana kipaji kama yeye na kwenda sehemu mbalimbali yeye binafsi au kwa kupitia taalum yake.” Ushauri wake kwa watu wote hasa wasichana anasema: “Fanya kazi yako sawasawa na taaluma yako itakulipa vyema.” Anawataka wanawake kuacha tabia ya kukaa bila kufanya kazi, badala yake anasema wanatakiwa kufanya kazi kwa bidii. Anaizungumziaje serikali ya awamu ya tano ya Rais Dk. John Pombe Magufuli hasa kuhusu Shirika la Ndege la Tanzania lililokufa kifo cha mende? “Ushauri wangu kwa serikali ni kwamba iwaruhusu wataalam wa sekta ya anga kutoka sehemu mbalimbali duniani kuja nchini na kufanya utafiti wa awali utakaojikita kwenye kulifufua upya shirika letu la ndege la taifa.” Anafadhaika akitulinganisha na nchi ya Rwanda ambayo imekuwa katika vita vya wenyewe kwa wenyewe kwa miaka mingi lakini sasa wametuzidi katika kuendesha shirika la ndege na sasa wanalo lao, Air Rwanda ambalo ndege zake husafiri hadi Dubai na kuunganisha hadi London Uingereza.
“Tanzania katika kipindi chote tangu tupate uhuru tumekuwa na amani lakini haiwezi kujivunia shirika lake la ndege kwa kutamba kuwa limekua,” anasema huku akiamini kuwa kuna watu waliliua shirika letu la ndege kwa manufaa yao binafsi.
Hata hivyo, hivi karibuni, Rais Dk. John Magufuli alionesha tumaini la kufufua shirika letu la ndege aliposema kwamba kutokana na ukusanyaji mzuri wa kodi za serikali, kuna uwezekano wa kununua ndege zetu hata kama itakuwa kwa awamu.
|
0 Comments