Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwezeshaji, Charles Mwijage
SEKTA binafsi katika nchi za Tanzania na Rwanda zimeonesha kuunga mkono jitihada za viongozi wa nchi hizo Rais John Magufuli na Paul Kagame za kuimarisha mahusiano ya kibiashara kwa kufanya mkutano wa kwanza wa Jukwaa la Biashara la Tanzania na Rwanda.

Mkutano huo utakaofanyika Mei 20, mwaka huu jijini Kigali, Rwanda unalenga kuwakutanisha wafanyabiashara na viongozi mbalimbali wa Serikali kwa ajili ya kujadili namna ya kuboresha mazingira ya kibiashara katika nchi hizo mbili.
Aidha, mkutano huo unatarajiwa kuja na mikakati ambayo itasaidia kusonga mbele na kuondoa vikwazo mbalimbali vilivyokuwepo kwa muda mrefu katika mahusiano ya kibiashara.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Meneja wa Jukwaa hilo, Hurbet Kissasi alisema, Rais Kagame atakuwepo katika tukio hilo pamoja na viongozi mbalimbali wa nchi hizo mbili kwa ajili ya kujadili mambo mbalimbali pamoja na wafanyabiashara hao.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Chama cha Wamiliki wa Malori nchini (TATOA), Emanuel Kikuyu alisema, sekta ya usafirisha ni moja ya sekta yenye mchango mkubwa katika pato la taifa.
Aliongeza kuwa Tanzania inazalisha bidhaa mbalimbali hivyo ni fursa nzuri kwa kuwa na soko jipya nchini Rwanda. Makamu Mwenyekiti wa Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo nchini (TCCIA), Dk Kingu Mtemi alisema, huduma za biashara, nishati na kilimo ni vipaumbele muhimu kwa nchi zote mbili.
Aidha, taasisi hizo za TATOA na TCCIA ambao ni waratibu wa jukwaa hilo kwa upande wa Tanzania wametoa mwito kwa wafanyabiashara kufika katika ofisi zao kwa ajili ya kujisajili kuhudhuria jukwaa hilo.