|
MADUDU mengi zaidi kuhusu watumishi hewa nchini yamebainika katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa ambako mishahara kwa watumishi waliofariki na waliotoroka ya jumla ya Sh bilioni 2.7 imelipwa katika mwaka wa fedha 2014/15.
Hayo yalielezwa katika Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ya mwaka 2014/15, Profesa Mussa Asaad aliyoiwasilisha bungeni mjini hapa jana. Katika ripoti hiyo, eneo la watumishi hewa, Profesa Asaad alisema udhaifu upo katika usimamizi wa rasilimali watu na taarifa za mishahara.
Alisema jambo hilo limekuwa sugu na Mamlaka ya Serikali za Mitaa inaongoza kwa kulipa mishahara watumishi waliofariki na waliotoroka kazini ya kiasi hicho cha Sh bilioni 2.7 kwa mwaka huo wa fedha wa 2014/15.
Profesa Asaad alisema Sh milioni 721 zililipwa kwenye mifuko ya hifadhi kwa watumishi hao ambao hawapo kazini tena, huku kwa upande wa Serikali Kuu, jumla ya Sh milioni 393 zililipwa kwa watumishi hewa.
Alibainisha kuwa Sh milioni 61 zililipwa kwenye mifuko mbalimbali ya hifadhi kama makato ya kisheria ya mishahara iliyolipwa kwa watumishi hao hewa. Ripoti hiyo ilibainisha kuwa jumla ya Sh bilioni mbili za mishahara haikulipwa kwa watumishi wa taasisi moja ya Serikali Kuu ambayo haikutajwa na kwamba fedha hizo pia hazikurudishwa Hazina.
CAG alisema Sh bilioni tatu zilizokuwa zimetengwa kwa watumishi wa Mamlaka ya Serikali za Mitaa 37, hazikuthibitishwa kurudishwa Hazina. Hali hiyo imeacha maswali mengi ya kuthibitisha fedha hizo zilikokwenda.
Kutokana na watumishi hewa, CAG ameshauri serikali iimarishe mifumo ya udhibiti wa ndani kuhakikisha orodha ya malipo ya mishahara inahakikiwa na makato ya kisheria yanawasilishwa kwa mifuko husika kwa wakati. Alishauri pia kiasi cha fedha za malipo ya mishahara ambayo haikulipwa kirudishwe Hazina.
Wakati CAG anabaini na kueleza hayo, nchi imekuwa katika kipindi cha uhakiki kwa watumishi wake baada ya Rais John Magufuli kuwaagiza wakuu wa mikoa kote nchini kufanya hivyo alipowaapisha Machi 15 mwaka huu, Ikulu, Dar es Salaam.
Uhakiki huo unaoendelea hivi sasa kote nchini, umebaini kuwapo kwa watumishi hewa zaidi ya 7,000 wanaosababisha hasara ya mabilioni ya fedha na baadhi ya mikoa ikiwamo Dar es Salaam, Kilimanjaro na Pwani imeiomba Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuchunguza suala hilo.
Rais John Magufuli, Aprili 21 mwaka huu alipozungumza na wenyeviti na makatibu wa CCM wa mikoa na wilaya za Tanzania na Visiwani, Ikulu, Dar es Salaam alisema kuna wafanyakazi hewa zaidi ya 7000. “Mpaka leo wafanyakazi hewa tuliowatoa kwenye ‘register’ wamezidi 7700 na bado uchambuzi unaendelea.
Sasa mnaweza mkaona kama kuna wafanyakazi hewa wa namna hiyo ndani ya serikali, hayo mabilioni ya fedha yangeweza kwenda kwenye huduma mbalimbali,” alisema Magufuli.
0 Comments