RAIS John Magufuli ameahirisha shamrashamra za maadhimisho ya siku ya Muungano na hivyo kuwezesha kuokoa zaidi ya Sh bilioni mbili, alizoagiza zikaanzishe upanuzi wa barabara inayokwenda Uwanja wa Ndege wa Mwanza.
Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu kwa vyombo vya habari kutoka Chato mkoani Geita ambako Dk Magufuli yuko mapumzikoni nyumbani kwake, Rais ameelekeza siku hiyo itakuwa ya mapumziko kama kawaida, na Watanzania waiadhimishe wakiwa majumbani kwao ama katika shughuli zao binafsi.
Sherehe za Muungano huadhimishwa kila Aprili 26 kusherehekea kuzaliwa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo ilianzishwa Aprili 26, 1964 baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
“Kufuatia kuahirishwa kwa shamrashamra hizo, Rais Magufuli ameelekeza kuwa fedha zilizopangwa kutumika kwa ajili ya kugharamia vinywaji, vyakula, gwaride, halaiki, burudani mbalimbali na hafla ya usiku ambazo ni zaidi ya shilingi bilioni mbili, zitumike kuanzisha upanuzi wa barabara ya “Mwanza - Airport” katika eneo linaloanzia Ghana Quaters hadi Uwanja wa Ndege wa Mwanza,” ilieleza taarifa ya Ikulu kutoka Chato.
“Barabara hiyo inafanyiwa upanuzi ili kukabiliana na kero ya msongamano mkubwa wa magari ambao unaathiri shughuli za kila siku za wananchi,” ilifafanua taarifa hiyo ya Ikulu.
Tangu aingie madarakani, Rais Magufuli alieleza azma ya Serikali yake ya Awamu ya Tano kubana matumizi na katika hatua alizochukua ni kufuta safari za nje ya nchi zisizo na tija, mikutano na makongamano, pamoja na kuahirisha sherehe mbalimbali na kuelekeza fedha zake katika masuala ya huduma za jamii.
Aliahirisha sherehe za Siku ya Uhuru, Desemba 9, mwaka jana na kutangaza siku hiyo kuwa ya kufanya usafi nchi nzima ili kukabiliana na ugonjwa wa kipindupindu katika dhana ile ya Uhuru ni Kazi.
Rais Magufuli aliagiza fedha zilizokuwa zitumike kwa sherehe hizo, Sh bilioni nne zikatumike kwa ajili ya upanuzi wa Barabara ya Bagamoyo kutoka Mwenge-Morocco, Dar es Salaam yenye urefu wa kilometa 4.3.
Aidha, Rais Magufuli alisitisha maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Kitaifa, ambayo yalikuwa yafanyike kitaifa mkoani Singida, Desemba mosi, mwaka jana.
Badala yake, aliagiza fedha zote ambazo zilitengwa na serikali pamoja na wahisani mbalimbali kwa ajili ya maadhimisho hayo, zielekezwe kununua vifaa tiba na vitendanishi. Serikali ilitenga kiasi cha Sh milioni 18 kwa ajili ya maadhimisho hayo huku kila mshiriki katika maonesho hayo akichangia kiasi cha Sh 500,000.
Awali Rais Magufuli aliagiza fedha zilizotengwa kwa ajili ya hafla ya uzinduzi wa Bunge zaidi ya Sh milioni 225, ziende kununulia vitanda kwa ajili ya wagonjwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dar es Salaam.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu mstaafu wa Kenya, Raila Odinga amerejea nchini Kenya baada ya kumaliza mapumziko yake ya siku tatu Lubambangwe katika Kijiji cha Mlimani, Wilaya ya Chato mkoani Geita alikomtembelea Rais Magufuli aliyepo mapumzikoni.
Akizungumza kwenye Uwanja wa Michezo wa Shule ya Sekondari ya Chato kabla ya kuruka kwa helikopta, Raila alimshukuru rafiki yake Rais Magufuli kwa kumpokea na pia aliwashukuru wananchi wa Chato kwa ukarimu wao kwa wageni.
Pia alisema ana imani kuwa Rais Magufuli ataisaidia Tanzania kukabiliana na changamoto mbalimbali, ikiwemo umasikini unaowakabili wananchi wake. “Lakini mimi najua yeye mwenyewe ana maono, anaona mbele na anajua yale ambayo yanatakiwa yafanyike ili Tanzania iinuke, itoke katika hali ya ufukara na kuwa katika hali ya maendeleo zaidi,” alisema Raila.
Raila na mkewe, Mama Ida Odinga waliwasili Chato, Jumamosi iliyopita kwa mapumziko na kuisalimia familia ya Rais Magufuli ambayo ni familia rafiki.
Katika hatua nyingine, Rais Magufuli ameahidi kutoa madawati na vitabu kwa wanafunzi wa shule tatu za msingi zilizopo Chato, ambao walijitokeza Uwanja wa Sekondari wa Chato wakati Rais Magufuli akimuaga mgeni wake Waziri Mkuu mstaafu wa Kenya, Raila Odinga.
|
0 Comments