|
SERIKALI kupitia Wizara ya Fedha na Mipango imefafanua kuwa Washirika wa Maendeleo bado wanaendelea kuisadia katika bajeti yake na kwamba tuhuma za kujitoa kwa makundi 14 ya kuisaidia bajeti sio za kweli.
Imesisitiza kuwa bado makundi hayo yanaendelea kuisaidia bajeti ya Tanzania, na kwa mwaka wa fedha 2015/2016, Washirika wa Maendeleo wanane waliahidi kuendelea kusaidia Bajeti Kuu wakiwemo Benki ya Maendeleo ya Afrika, Canada, Denmark, Umoja wa Ulaya, Finland, Ireland, Sweden na Benki ya Dunia.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dk Servacius Likwelile, kwa mwaka wa fedha 2016/2017 baadhi ya Washirika wa Maendeleo wameshathibitisha kusaidia Bajeti Kuu ya Serikali. Aliwataja kuwa ni pamoja na Benki ya Maendeleo ya Afrika, Denmark, Umoja wa Ulaya pamoja na Benki ya Dunia.
Wengine watakaoendelea kuisaidia Serikali kupitia wa Mfuko wa Pamoja wa Maendeleo na Miradi. Hao ni pamoja na Ubelgiji, Canada, China, Denmark, Finland, Ufaransa, Ujerumani, Hispania, India, Italia, Japan, Korea Kusini, Norway, Sweden, Uholanzi, Uingereza, Marekani na Uswisi.
Washirika wengine wa maendeleo ambao wanaisaidia bajeti ya Serikali ni Benki ya Maendeleo ya Afrika, Mashirika ya Umoja wa Mataifa, BADEA, Mfuko wa OPEC pamoja na Saudi Arabia, Umoja wa Ulaya na Benki ya Dunia.
Taarifa hiyo ya Dk Likwelile iliongeza kuwa Serikali ya pamoja na Washirika wa Maendeleo wanaoisaidia Tanzania wako katika mazungumzo juu ya namna ya kuimarisha ushirikiano wa kimaendeleo kati ya Tanzania na nchi hizo.
“Serikali imewashukuru Washirika wa Maendeleo kwa kuendelea kuisaidia Tanzania katika kupelekea juhudi za kimaendeleo zenye tija kwa wananchi,” alisema Dk Likwelile.
0 Comments