RAIS mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa amesema viongozi wote wanawajibika kuishi kwa mfano wa aliyekuwa Waziri Mkuu, Hayati Edward Sokoine aliyejitoa kutumikia taifa huku akimtaja Rais John Magufuli ametokana na kuishi namna hiyo.
Alisema hayo juzi baada ya misa takatifu ya kumkumbuka Sokoine iliyofanyika katika Kanisa Katoliki, Parokia ya Mtakatifu Joseph jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa pia na Rais John Magufuli.

Mkapa alisema mfano huo wa Sokoine, ndio ulioiwezesha Tanzania kumpata kiongozi wa sasa, Rais John Pombe Magufuli anayetaka kuonesha misingi ya uongozi bora, uadilifu, kusimamia amani, utulivu na maendeleo.
Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo alimpongeza Rais Magufuli kwa kufuata nyayo za Sokoine katika kuliongoza Taifa.
“Kuna baadhi ya watu wanasema Rais wetu wa sasa ni sura ya Edward Moringe Sokoine,” alisema Pengo, na kumtaka Rais Magufuli na serikali yake kusonga mbele na kujenga heshima ya nchi. Pengo alisema Sokoine hakuwa kiongozi wa kujiangalia yeye, bali alikuwa ni kwa ajili ya watu.
Kwa upande wake, Rais Magufuli amewasihi Watanzania kuendelea kushikamana, kupendana na kuenzi mazuri yaliyofanywa na viongozi wa taifa waliotangulia mbele ya haki, akiweno aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Sokoine.
Akizungumza baada ya misa hiyo, Magufuli alihimiza Watanzania kuenzi mazuri yote yaliyofanywa na viongozi wengine waliotangulia mbele ya haki, hususani Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Amaan Karume, Magufuli alisema kazi nzuri ya mtu huwa haipotei.
Alisema anamkumbuka Sokoine alivyokuwa kiongozi shupavu, aliyewapenda watanzania, aliyependa kuwatumikia watanzania, mchapakazi, aliyechukia rushwa, aliyechukia ufisadi na aliyechukia uonevu kwa watu wa chini.
“Namuona (Sokoine) ni kielelezo cha pekee katika Taifa letu la Tanzania, miaka 32 iliyopita wakati Mzee wetu Edward Moringe Sokoine alipoitwa na kutangulia mbele ya haki, wakati huo mimi nilikuwa JKT Mpwapwa, ninaikumbuka siku hiyo ilikuwa ya majonzi makubwa,” alisema.
Sokoine alifariki dunia miaka 32 iliyopita, kwa ajali ya gari katika eneo la Dakawa wakati akitokea Bungeni Dodoma.
Misa ya kumkumbuka ilihudhuriwa pia na Mke wa Rais Mama Janeth, Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin William Mkapa na familia ya Sokoine.