Kaimu Kamanda wa Mkoa wa Shinyanga, Dismas Kisusi
MJI wa Kahama mkoani Shinyanga juzi ulisimamisha shughuli zake kwa takribani saa tatu kutokana na majambazi waliovamia duka na kuua mjini hapa, kurushiana risasi na polisi; tukio lililosababisha vifo vya watu watano.
Uvamizi huo ulifanyika saa 12 jioni kwenye duka la Emanuel Mkumbo na baada ya kukosa fedha, walimuua mfanyabiashara huyo na mtu mwingine kwa kuwapiga risasi.

Wakati wakikimbia, polisi iliwadhibiti ndipo wakaanza majibizano ya risasi yaliyodumu kwa takribani saa tatu kabla ya kuua majambazi watatu.
Kaimu Kamanda wa Mkoa wa Shinyanga, Dismas Kisusi alisema polisi walifanikiwa kuwanyang’anya majambazi hao bunduki moja ya kivita aina ya SMG (uzgun), kisu kimoja cha kijeshi na bomu moja la kutupa.
Kisusi alithibitisha watu watano kupoteza maisha katika tukio hilo na kwamba miongoni mwao, watatu ni hao majambazi waliokuwa wakirushiana risasi na polisi.
Mmoja wa majambazi hao waliouawa, ametambulika ni Zacharia Yona na wengine wawili hadi jana walikuwa hawajafahamika.
Kwa upande wa raia waliopoteza maisha, licha ya mfanyabiashara Mkumbo ambaye ni mkazi wa Mkoa wa Singida, mwingine ni dereva wa lori aina ya Fuso aliyekuwa ameegesha gari lake pembeni ya barabara, akishuhudia mapambano kati ya polisi na majambazi.
Baadhi ya wakazi wa Mji wa Kahama, walilipongeza jeshi la Polisi kwa kufanikisha kupambana na majambazi hao. Ilielezwa kwamba, ndani ya wiki moja iliyopita, ulifanyika uvamizi kwa maduka manne mjini hapa na kupora fedha nyingi.
“Tulikuwa tukifanya biashara zetu hadi saa kumi na moja jioni na kisha tunafunga kutokana na hali ya wasiwasi iliyokuwa imetanda baada ya majambazi kufanya matukio manne mfululizo hapa mjini. “Na ukiangalia muda huo ndio muda wa kufanya biashara na majambazi ndio hao,” alisema mmoja wa wafanyabiashara ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini.
Rais Magufuli alipokuwa akiapisha wakuu wa mikoa mwezi uliopita, miongoni mwa mambo aliyowataka wasimamie ni pamoja na kukabili ujambazi.
Aliwataka wakuu wa mikoa husika, kuhakikisha wanakomesha vitendo hivyo ili wananchi wakae kwa amani hususani katika mikoa ya pembezoni, ambayo imekuwa ikiwalazimu polisi kusindikiza mabasi ya abiria kwa hofu ya kutekwa.