Paul-Makonda (1)Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda
Stori: Richard Bukos, Risasi Jumamosi
Dar es Salaam: Ile amri ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ya kutaka kumbi zote za starehe kufungwa inapofika saa sita za usiku, imemwangukia Mkurugenzi wa Bendi ya African Stars ‘Twanga Pepeta’, Asha Baraka baada ya juzikati polisi walioambatana na maafisa wa serikali kuvamia onesho la bendi yake.

Sakata hilo lilitokea mishale ya saa nane za usiku, kwenye Ukumbi wa Mango Garden, Kinondoni jijini hapa ambapo bendi hiyo ilikuwa ikiendelea kupiga shoo na kutoa tuzo kwa wadau wake lakini ghafla wakaingia askari kadhaa wakiwa na silaha sambamba na maafisa hao na kuamuru muziki uzimwe.
ashaAsha Baraka
“Unaambiwa ulikuwa ni mtiti wa nguvu, Asha Baraka akawa hataki muziki uzimwe kwa sababu mashabiki waliolipa viingilio wasingemuelewa, wangeweza hata kuharibu vyombo vyake vya muziki,” alisema shuhuda mmoja wa tukio hilo na kuongeza:
“Maofisa hao walimwambia Asha Baraka kuwa walikuwa wakitekeleza agizo la Mkuu wa Mkoa wa Dar, Makonda la kumbi zote za burudani kufungwa saa sita kamili vinginevyo kuwe na kibali maalum. Walivutana kwa muda mrefu sana.”
Hata hivyo, baada ya majadiliano yaliyochukua muda mrefu, maafisa hao na polisi waliondoka na kuacha burudani ikiendelea lakini walimuonya Asha Baraka kwamba akirudia kuvunja sheria ‘atakiona’.
Akizungumza na mwandishi wetu kuhusu tukio hilo, Asha Baraka alisema: “Ni kweli kibali changu hapa kinaonesha inatakiwa tufunge saa sita lakini wakati mwingine mashabiki wanakuwa wagumu kuelewa, wanaweza kusababisha vurugu,” alisema.