WAZIRI wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amewasili nchini kutoka Kampala, Uganda na kusema miundombinu ya Tanzania na usalama wake ni moja ya mambo yaliyowezesha Tanzania kupata dili la ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Hoima, Uganda hadi bandari ya Tanga.
Akizungumza na waandishi wa habari mara tu baada ya kuwasili jana jioni alisema kwamba maunganiko ya reli ya Tanga hadi reli ya Kati na uwapo wa barabara kumeipatia Tanzania nafasi ya ujenzi wa bomba hilo kwani kaskazini mwa Kenya miundombinu hiyo haipo.
Akizungumza huku akimfagilia Rais John Magufuli kwa kazi yake nzuri ya kusimamia ujenzi wa barabara wakati alipokuwa Waziri wa Ujenzi, alisema kama kungelikosekana miundombinu hiyo kungeliikosesha Tanzania mradi huo muhimu Afrika Mashariki.
Tanzania ilikuwa inashindana na Kenya katika kupata nafasi ya kutekeleza mradi huo wenye kilomita 1,403 utakaobeba mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Tanga. Mradi huo wa dola za Marekani bilioni 4 sawa na Sh trilioni 8.7 ni ushindi mkubwa kwa Watanzania ambao walipeleka Uganda timu ya wataalamu kuwezesha ushawishi wa kwa nini Bomba hilo la mafuta linafaa kupitia Tanzania.
Kwa mujibu wa Waziri Muhongo mradi huo utakamilika Juni 2020 na kwamba mkutano wa Mawaziri wa Tanzania na Uganda wa Nishati na Madini na wataalamu wao kuhusiana na mpango wa utekelezaji utafanyika Ijumaa ijayo mjini hapa.
Pamoja na kuwapo kwa Waziri wa Nishati na Madini wa Uganda, Irene Muloni, ambaye ataongoza ujumbe kutoka Uganda kutakuwapo pia wajumbe kutoka kampuni mbalimbali zikiwemo Total E&P ya Ufaransa, Tullow Oil ya Uingereza na China National Offshore Oil Corporation na Kampala.
“Katika mkutano huu tutatengeneza mpango kazi wa mradi na mkutano huo utahudhuriwa pia na kampuni wadau wa ugunduzi wa mafuta nchini Uganda,” alisema. Profesa Muhongo alisema lengo ni kuanza ujenzi huo haraka kuliko lilivyojengwa bomba la gesi toka Mtwara hadi jijini Dar es Salaam ili lianze kazi Juni 2020 na kuwa zawadi kwa Rais Magufuli kabla hajachukua fomu kwa ajili ya uchaguzi wa mwaka huo.
Aidha Muhongo alimpongeza Rais Yoweri Museveni wa Uganda kwa kufanya maamuzi ya kupitisha bomba Tanzania kwa kuzingatia ubora wa bandari na njia inayopita bomba hilo la mafuta. Profesa Muhongo alisema kulikuwa na ushindani wa aina mbili wa ubora wa bandari na njia ambapo bomba litajengwa kulikuwa na ushindani wa bandari ya Tanga, Lamu na Mombasa lakini mambo yalipokuwa magumu waliitoa bandari ya Mombasa.
Alisema ikabaki mapambano ya Lamu na Tanga na wataalamu wa Tanzania toka sehemu mbalimbali walieleza ubora wa bandari ya Tanga kuwa na kina kirefu kuliko Lamu na Mombasa na hata bandari nyingine nchini. Alisema bandari hiyo iko mita 23 ambazo zinatakiwa kimataifa na meli kubwa zinaweza kutia nanga na kupakia mzigo.
Aidha alisema sababu nyingine ni hali ya tambarare iliyopo ambako bomba la mafuta litapita tofauti na Kenya kwenye mabonde na milima ambapo kunaingia gharama kubwa ya mashine za kusukuma mafuta. Kuwapo kwa bomba hilo kutasaidia pia mataifa ya Kenya, Sudan Kusini, Rwanda, Burundi na Congo (DRC).
“Itakuwa rahisi kwa mataifa haya kutumia bomba hili la mafuta ukilinganisha bandari yoyote ile Afrika Mashariki, kiukweli njia ya Tanzania ni rahisi inayoaminika na salama,” alisema Profesa Muhongo. Bomba hilo lenye kipenyo cha inchi 24 litakuwa na urefu wa kilomita 1,403 na linatarajiwa kusukuma mapipa 200,000 kwa siku.
Kuwepo kwa mradi huo kutatengeneza ajira kwa watu elfu 15 na ujenzi ukimalizika kutakuwapo n ajira kati ya watu 1000 na 2000. Aidha magari ya kusomba mizigo zaidi ya 100,000 yatakuwa kazini huku wafanyabiashara wakipata fursa mbalimbali za biashara wakati wa ujenzi.
Bomba hilo likiingia Tanzania litapita mikoa ya Kagera, Geita, Shinyanga, Tabora , Singida hadi Tanga. Uganda imegundua mafuta yanayofikia mapipa bilioni 6.5 katika Ziwa Albert. Mchakato ulivyokuwa Awali, serikali za Uganda na Kenya, ziliwahi kufikiria kupitisha bomba hilo katika ardhi ya Kenya, kwa nia ya kutumia bandari itakayojengwa ya Lamu nchini humo.
Hata hivyo, wakati hatua za kina hazijachukuliwa, Rais wa Tanzania, Dk John Magufuli na Rais Museveni walikutana mwanzoni mwa mwezi uliopita na baada ya mazungumzo yao, wakatoa agizo kuwa mchakato wa ujenzi wa bomba hilo, ufanyike kwa kasi.
Baada ya kikao cha marais hao kutoa agizo hilo, kilifuata kikao cha Rais Magufuli na Makamu wa Rais wa Kampuni ya Total, tawi la Afrika Mashariki, Javier Rielo, ambapo kiongozi huyo wa kampuni alimhakikishia Rais Magufuli kuwa kampuni yao itaanza ujenzi wa bomba hilo haraka iwezekanavyo, kwa kuwa fedha za kutekeleza mradi huo zipo.
Katika mazungumzo hayo, Rielo alimueleza Rais Magufuli kuwa kampuni yake inatarajia kutumia Dola za Marekani bilioni 4 ambazo tayari zimeshaandaliwa. Makubaliano ya awali Katika utekelezaji wa agizo la Rais Magufuli na Rais Museveni, Machi 17 mwaka huu, serikali za Tanzania na Uganda pamoja na kampuni ya Total E&P Uganda na Shirika la Maendeleo ya Petroli la Tanzania (TPDC), walitia saini mpango wa pamoja wa utekelezaji wa mradi huo.
Mpango huo ulitiwa saini na Waziri wa Nishati na Madini wa Tanzania, Profesa Muhongo; Waziri wa Maendeleo ya Nishati na Madini wa Uganda, Irene Muloni; Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Dk James Mataragio na Meneja Mkuu wa Total E&P Uganda, Adewale Fayemi.
Malumbano Baada ya utekelezaji wa agizo hilo kufikia hatua ya mkataba kuliibuka mjadala kuhusu uhakika wa bomba hilo kupita Tanzania baada ya Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta kukutana na Rais Museveni, kujaribu kuangalia uwezekano wa bomba hilo kupitia Kenya kwenda Lamu.
Pamoja na jitihada hizo, Bandari ya Tanga, ilibakia kuwa eneo pekee lenye mazingira bora, nafuu na yenye ufanisi kwa utekelezaji wa mradi huo. Uzoefu Mbali na Bandari ya Tanga kuwa ya kimkakati zaidi katika utekelezaji wa mradi huo, Tanzania ndiyo yenye uzoefu wa muda mrefu na wa hivi karibuni wa ujenzi, uendeshaji, ulinzi na uelimishaji jamii katika miradi ya bomba la mafuta.
Uzoefu ni wa ujenzi, uendeshaji na uhudumiaji wa Bomba la Mafuta la Tanzania na Zambia (Tazama) tangu mwaka 1968, likitoka Dar es Salaam mpaka Ndola Zambia. Bomba hilo lenye kipenyo cha nchi 8 mpaka 12 na urefu wa kilometa 1,710; kati ya hizo kilometa 860 zipo kwenye ardhi ya Tanzania na limekuwa likipitisha mafuta tani milioni 1.1 kwa mwaka.
|
0 Comments