MAKAMANDA wa Polisi, mikoa ya Kipolisi Dar es Salaam wameanza harakati za kukabiliana na wimbi la uhalifu wa kutumia silaha lililoibuka siku za karibuni. Katika mahojiano na gazeti hili pamoja na kuthibitisha kuwapo kwa wimbi hilo wameuhakikishia umma kuwa hatua za makusudi zinafanyika kubaini mtandao huo na kuufuta.

Katika siku za karibuni maeneo mbalimbali ya mkoa wa Dar es Salaam yamekumbwa mfululizo na uvamizi katika makazi ya watu na biashara. Maeneo ambayo gazeti hili limebaini kuwapo matukio mengi ya ujambazi, ni katika wilaya ya Kinondoni ambako uvamizi huo umeambatana na mauaji kwa raia.
Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Kinondoni, Christopher Fuime, alithibitisha kuwepo kwa matukio ya ujambazi katika maeneo mbalimbali ambayo hata hivyo alisisitiza kuwa hatua zinachukuliwa kuyadhibiti. Mbezi Fuime alizungumzia tukio la ujambazi la hivi karibuni katika eneo la Mbezi Msumi ambako maduka kadhaa yalivamiwa na majambazi waliokuwa na silaha aina ya shot gun.
“Kwa bahati mbaya wakati wakifyatua risasi hewani, maganda ya silaha ile, yalimpata kijana mmoja aliyekuwa amekaa pembeni akinywa kahawa ambaye alipoteza maisha,” alisema Kamanda Fuime. Alisema katika tukio hilo, majambazi hao walipora kwenye maduka hayo kiasi cha fedha kati ya Sh 150,000 na 250,000. Aidha, alisema miezi kadhaa iliyopita , katika eneo la Salasala kulitokea ujambazi ambao aina ya silaha iliyotumika (shot gun) inasadikiwa ndiyo ilitumika kwenye tukio la Mbezi Msumi.
“Tunajua huu ni mtandao, tumeweka mkakati wa kuusambaratisha na kwa sasa tunaitafuta bunduki hii, ndiyo itatusaidia kuwapata majambazi hawa,” alisema Kamanda wa Polisi. Kamanda Fuime alisema Polisi imeimarisha ulinzi hasa katika maeneo ya pembezoni ya mji, ambayo yamebainika ndiyo yamekuwa yakishambuliwa na wahalifu.
Maeneo mengine ambayo ulitokea uvamizi uliosababisha kifo cha raia, ni pamoja na kata ya Kibamba ambako wiki iliyopita nyumba nne zilivamiwa kwa mpigo katika mtaa wa Kibwegere na kusababisha kifo cha mkazi wa eneo hilo, Julias Sillambi (56).
Eneo lingine ambalo linatajwa kukumbwa na wimbi la uvamizi hivi karibuni, ni Mbweni ambako Katibu wa Ulinzi wa eneo la Mbweni Teta, Mgina Mfaume, alisema takribani matukio 48 ya uvamizi yamejitokeza kuanzia Juni 26 mwaka jana hadi mwezi huu .
Alisema kati ya matukio hayo, 16 yameripotiwa rasmi Polisi kituo cha Wazo na takribani matukio 32 hayajaripotiwa. Ulinzi shirikishi Wakizungumza na gazeti hili, wananchi sanjari na polisi, wameshauri dhana ya ulinzi shirikishi ipewe msukumo.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Fuime alitoa mwito kwa wananchi kwa kushirikiana na Serikali za mitaa, kuanzisha vikundi vya ulinzi shirikishi. Kwa upande wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Lucas Mkondya, akizungumzia hali hiyo ya ujambazi, alisema wameimarisha doria hasa katika maeneo ya pembezoni na miji mipya ambayo ndio maeneo yanayovamiwa zaidi na majambazi.
“Tunajitahidi kufanya msako na doria usiku na mchana lakini kwa kuwa sisi ni wachache na hatuwezi kufikia maeneo yote, kila mtaa wameunda vikundi vya ulinzi shirikishi na kila kata wamepeleka askari kwa ajili ya kusaidiana na vikundi hivyo,” alisisitiza.
Wakati huo huo katika mikoa mbalimbali, Polisi imesema imeimarisha ulinzi, doria na misako dhidi ya majambazi ikiwa ni pamoja na kufufua mfumo wa kutumia askari kata, ambao watashirikiana na wananchi kwa siri kubaini na kuripoti matukio ya uhalifu.
Arusha Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas alisema mkoani humo, wamefanikiwa kupunguza matukio ya ujambazi kutokana na kushusha madaraka ya ulinzi mikononi mwa wananchi.
“Kuna msemo usemao, mchawi mpe mwanao alee, ndio na sisi tunatumia wananchi kuwapa madaraka, wao ndio wanawajua hawa wahalifu hivyo wakishiriki katika masuala ya ulinzi katika maeneo yao ni rahisi kupata taarifa za wahalifu na kudhibiti matukio,” alisisitiza.
Aliwataka wananchi watambue kuwa jukumu la ulinzi si la Polisi pekee bali ni la Watanzania wote. Njombe Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Prudensiana Protas alisema wameimarisha msako, ulinzi na doria sambamba na kutoa elimu kwa jamii ya jinsi ya kukabiliana na majambazi.
Mbeya Kwa upande wake, Mkuu wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ahmed Msangi alisema mkoa wake unapambana na uhalifu wa kutumia silaha kwa kujikita katika kupokea taarifa ili kudhibiti kabla ya tukio halijafanyika.
Alisema hupata taarifa za mipango ya wahalifu kutoka kwa wananchi, askari kata na tarafa na viongozi wa makabila kama machifu. Msangi alisema pia wamekuwa wakifanya msako na doria za kila siku na kuhamasisha kuanzishwa kwa makundi ya ulinzi na ulinzi shirikishi. Geita Mkuu wa Polisi Mkoa wa Geita, Mponjoli Lotson alisema wameunda kikosi kinachojumuisha mikoa minne ya Geita, Mwanza, Kagera na Kigoma cha kupambana na uhalifu.
Manyara Mkoani Manyara, Kamanda wa Polisi , Francis Massawe alisema pia wao wameweka mikakati ya kukabili uhalifu kabla haujatokea. Alisema tatizo kubwa lilikuwa likijitokeza kwenye minada hususan mnada unaofanyikwa eneo la Sunya, Kiteto.
Alisema Polisi imekuwa ikituma askari kwenye minada hiyo. Alisema pia wanafanya doria za kawaida na kutumia Kikosi cha Intelijensia kwa ajili ya kupata taarifa na kutumia wananchi na Polisi Jamii.