Raia 13 wa Rwanda wamekuwa wa kwanza kurejeshwa Kigali kufuatia kutibuka kwa ghasia dhidi yao nchini Zambia.
Serikali ya Rwanda imechukua hatua hiyo kufuatia ghasia zilizowalenga wanyarwanda na biashara zao nchini Zambia.

Waliorejea nchini Rwanda ni watu 13 walioweza kufika kwenye afisi za ubalozi wa Rwanda mjini Lusaka na ambao mali zao iliteketezwa kabisa.
Katika mazungumzo na BBC wanyarwanda hao wanasema mali zao nchini Zambia ziliteketezwa na kwamba hali ya maisha nchini Rwanda itakuwa ngumu kwa kuwa walikuwa wameishauza mali zao kabla ya kuwekeza nchini Zambia.
Mmoja wa wanyarwanda hao Alfani Sindaheba amesema kuna uhasama na chuki dhidi ya wageni Zambia.
Ameongeza kuwa sababu nyingine inaweza kuwa ya kisiasa hasa mbinu za wapinzani kutaka kumharibia sifa rais Edgar Lungu.
Image copyright
Image captionPolisi walikuwa na wakati mgumu kudumisha hali ya amani
“mwezi wa 8 kutafanyika uchaguzi na huyu rais baadhi hawampendi kwa sababu alipofika madarakani alibadilisha mambo mengi na dolla ya Marekani ikapanda sana,hivyo wengi hawakupendezwa na mageuzi aliyoyafanya.'
''Nafikiri baadhi ya wanasiasa wametumia machafuko haya ya chuki dhidi ya wageni kutaka kumvuruga rais Lungu.”alisema Bwana Sindaheba.
Wanyarwanda hao waliorejea kutoka Zambia baadhi wamesafirishwa katika maeneo yao asilia na wengine wamesalia hotelini mjini Kigali,wakisubiri mipango ya serikali ya kuwasafirisha hadi mikoa yao asilia.