Mkurugenzi Mtendaji wa Kilombero Sugar Mark Bainbridge akiwaongoza Wazazi na wafanyakazi wa Kilombero Sugar kukagua darasa katika shule ya msingi Muungano lililojengwa kwa ufadhili wa chama cha kusaidia jamii cha Kilombero Community Charitable Trust (KCCT). Hafla hiyo ilifanyika Kilombero mwishoni mwa wiki.
 Mkurugenzi mtendaji wa Kilombero Sugar Mark Bainbridge akiwa katika picha ya pamoja na wanafunzi wa shule ya msingi ya Muungano mbele ya darasa la awali lililojengwa kwa ufadhili wa chama cha kusaidia jamii cha Kilombero Community Charitable Trust (KCCT) Hafla hiyo ilifanyika Kilombero mwishoni mwa wiki.
Mwakilishi wa Kilombero Sugar Joseph Rugaimukamu akiwa na wanafunzi wa shule ya msingi Muungano baada ya kukabidhiwa madawati na chama cha kusaidia jamii cha Kilombero Community Charitable Trust (KCCT), hafla hiyo ya kukabidhi ilifanyika mwishoni mwa wiki mkoani Morogoro. 
******************
Kiwanda cha Sukari cha Kilombero kimewekeza zaidi ya shilingi milioni 200 katika kipindi cha mwaka jana kutekeleza miradi mbalimbali ya kijamii katika nyanja za afya na elimu, ikiwa ni kurudisha sehemu ya pato lake kwa jamii ambapo kiwanda kinaendesha shughuli zake.

Meneja wa Mfuko wa kusaidia Jamii (Kilombero Community Charitable Trust (KCCT) Mary Elizabeth alisema jana kuwa miradi iliyotekelezwa mwaka jana ni pamoja na ujenzi wa madarasa miwili katika shule za msingi Kalunga na Muungano kwa jumla ya shilingi milioni 38.5.

Alisema kabla ya utekelezaji wa mradi huu, wanafunzi wa chekechea walikuwa wakisomea chini ya mti wa mwembe ambapo masomo yamekuwa yakiahirishwa mara kwa mara kutokana na mvua na wakati mwingine ilibidi kufyeka majani marefu ili kuandaa sehemu ya kusomea.

Mradi mwingine uliotekelezwa ni pamoja na ujenzi wa vyoo katika shule za msingi Mang’ula and Mgudeni wenye thamani ya shilingi milioni 30. Kila choo kina mashimo sita na sehemu ya kujisaidia haja ndogo na pia kwa ajili ya watu wenye ulemavu.

 “Pamoja na kuwa Mmoja wa wazalishaji wakubwa wa Sukari nchini, pia Kiwanda cha Sukari Kilombero kimekuwa mstari wa mbele kusaidia miradi mbalimbali ya afya na Elimu ili kuweza kuboresha mazingira ya kusomea and afya za Watoto wa wilaya za Kilombero na Kilosa,” alisema.

Aliitaja miradi mingine ya kijamii iliyotekelezwa ikiwa ni Pamoja na ujenzi wa bweni la wasichana katika shulie ya sekondari ya Ruhembe kwa thamani ya shilingi milioni 90 ambalo litaweza kupokea wanafunzi 48. Hii itaondoa usumbufu wa kutembea kwa zaidi ya kilomita 40 kila siku kwa wasichana hawa.

Kwa upande wa afya, Kiwanda cha Sukari Kilombero kinaendelea na ujenzi wa Nyumba ya wafanyakazi wa afya katika hospitali ya Nyandeo wenye thamani ya shilingi milioni 43. Pia katika kuendeleza mashirikiano kati ya Mfuko wa Kusaidia Jamii na Kiwanda cha Sukari wamewekeza zaidi ya shilingi milioni 700.

Akishukuru katika hafla ya makabidhiano, mkuu wa shule ya sekondari ya Ruhembe Bw Johannes Ruekulamu alishukuru Kiwanda cha Sukari Cha Kilombero kwa ujenzi wa bweni ambalo litaongeza ufaulu, nidhamu na kupunguza mimba kwa Watoto wa shule.

Naye mwenyekiti wa kamati ya Wazazi shule ya msingi Muungano Bw Denis Athanas alisema ujenzi wa madarasa utamaliza kabisa tatizo la muda wa zaidi ya miaka sita ambapo wanafunzi wamekuwa wakisomea chini ya mti na mara nyingi wakinyeshewa na mvua au jua kali.