Uganda imeamua kujenga bomba la mafuta yake kupitia Tanzania na wala sio Kenya.
Awali taifa hilo la Afrika mashariki ambayo haijapakana na bahari ilikuwa imezungumzia nia ya kujenga bomba la mafuta yake kupitia Kenya lakini baada ya mkutano na rais wa Tanzania Joseph Pombe Magufuli, rais wa Uganda Yoweri Museveni wameibwaga Kenya.
Kenya ambayo imegundua mafuta Kaskazini mwa taifa hilo sasa haina budi kujiunga na uganda kupitishia mafuta yake Tanzania au ijenge bomba lake kupitia bandari ya Lamu.
Uganda imeelezea wasiwasi wa mabomba ya mafuta kushambuliwa na wanamgambo wa Alshabab kwani bomba hilo la kupitia Kenya linatazamiwa kutumia bandari ya Lamu.
Uganda ilitangaza uamuzi wake katika kongamano la viongozi wa muungano wa Afrika Mashariki uliokuwa mji mkuu wa Kampala.
Muungano huo unajumuisha Kenya, Tanzania, Burundi, Rwanda na Sudan Kusini.
Bomba hilo la mafuta litakwenda kilomita 1,400km kuanzia Hoima, hadi kwenye bandari ya Tanga.
Mradi huo utagharimu takriban dola bilioni $4 za Marekani.
Aidha ujenzi huo unatarajiwa kutoa nafasi za kazi 15,000 kwa vijana ambao wanatatizika sana na uhaba wa ajira.
Uganda inakisiwa kuwa na mapipa bilioni 6.5 bn ya mafuta yanayotarajiwa kuanza kuchimbwa mwaka wa 2018.
Kampuni ya mfuta ya Ufaransa Total, ile ya China CNOOC na ile ya Uingereza Tullow ndizo zinazomiliki leseni ya kuchimba na kusafisha mafuta nchini Uganda.
Kenya sasa imeamua kujenga bomba lake kufuatia uamuzi huo wa Uganda.
0 Comments