Waziri Mkuu mstaafu, Joseph Warioba
WAZIRI Mkuu mstaafu, Joseph Warioba amesema Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana (2015) ulifanyika kwa haki huku akitaka vyama vya siasa kuwa na demokrasia ndani yao, kuhakikisha wanayotaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) iwafanyie, wao pia wayafanye kwenye vyama vyao.

Amesema nchi inatakiwa kuangalia na kujadili uchaguzi usiwe bidhaa inayotafutwa kwa fedha kama ambavyo ilijitokeza katika uchaguzi wa mwaka jana ambao rushwa ilitumika kwa kiwango kikubwa.
Akizungumza katika mdahalo wa kitaifa kuhusu uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka jana, Warioba pia ametoa angalizo kwa asasi za kiraia kuwa makini na wafadhili wao kuepuka kuingiza matakwa yao (wafadhili) kwenye siasa za ndani.
Mdahalo huo uliofanyika jana jijini Dar es Salaam, ulioandaliwa na Mpango wa Elimu ya Demokrasia Tanzania (REDET) na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, (LHRC).
Akiwasilisha mada, Warioba ambaye amepongeza utendaji wa Rais John Magufuli, alisema uchaguzi mkuu ulikuwa na hamasa ambayo haijapata kutokea lakini ulikuwa huru na ulimalizika kwa amani na utulivu .
Alisema akiwa mmoja wa waangalizi aliyewahi kusimamia chaguzi za Zambia, Malawi, Nigeria, Ghana, Ethiopia na Sudan, anafahamu masuala ya uangalizi na kutoa ripoti. Alisema ni kweli uchaguzi ulienda vizuri. Alisema alipoangalia maoni ya waangalizi wa nje alishangaa kwa mara ya kwanza kusifu mchakato mzima wa uchaguzi.
Alisema licha ya kuwapo kwa upungufu mdogo, waangalizi hao walisifu mchakato mzima na zaidi alishangaa kuona waangalizi ambao wagumu kusifia ; mfano Umoja wa Ulaya (EU), waliridhishwa na uchaguzi huo.
Vyama, asasi vyamulikwa
Hata hivyo alisema, katika kukuza demokrasia kwenye vyama, yapo matatizo na ipo kazi ya kufanya kwa kuwa rushwa imekuwa ikitumika kwa kuwepo matumizi mabaya ya madaraka.
Alisema bila kuleta demokrasia ndani ya chama, ni vigumu kufanikiwa katika kukuza demokrasia nchini.
“Ni rahisi kulaumu Tume ya Uchaguzi (NEC) lakini ndani ya vyama hawafuati yale wanayotaka NEC iwafanyie hivyo lazima kuwe na demokrasia ndani ya chama kwani kukiwa na vyama bila demokrasia hatupati nchi yenye demokrasia hivyo wanasiasa tupige kelele ndani ya vyama siyo NEC,”alisisitiza.
Kwa upande wa asasi za kiraia kuwa walifanya kazi ipasavyo lakini alishauri elimu kwa mpigakura iwekwe kwenye mtaala wa shule nchini na isisubiri kutolewa wakati wa uchaguzi.
Asasi na wafadhili
Akizungumzia nafasi ya asasi za kiraia, alisema zipo baadhi katika kutoa elimu, ziligeuka wanaharakati na kufikia kuhamasisha wachague chama au mgombea yupi .
Alisema walifanya hivyo ikidaiwa ni matakwa ya wafadhili jambo alilosema kwamba ni hatari masharti ya wafadhili kuingilia siasa za nchi.
Wanahabari
Jaji Warioba alizungumzia pia ushiriki wa vyombo vya habari katika uchaguzi huo na kusema vyote vilikuwa na upendeleo. Alisema hata magazeti yaliyosifika kwamba hayana upendeleo, yalizidi na mpaka sasa vyombo hivyo vina upande wake.
Alitaja baadhi ya mambo ya kuboresha ni mfumo wa kisheria na kitaasisi kwa kuboresha katiba kukuza demokrasia.
Alisema ushindi wa rais uhojiwe mahakamani na kuwepo kwa kura za uwiano kwa wabunge kuleta usawa wa kijinsia pamoja na vyama vidogo vya siasa kukua.
NEC kulalamikiwa
Alisema lazima kuwa na tume inayoaminika na wote ambayo haitawekwa wanasiasa.
Akizungumzia suala la gharama za uchaguzi,Warioba alisema sheria ipo lakini haitekelezwi kwani vyama vikubwa vinapata faida kuliko vidogo .
Alisema uchaguzi mkuu wa mwaka jana ulikuwa ni wa fedha hivyo kugeuka bidhaa kwa wenye fedha kushinda.
Alisema athari zilizojitokeza katika uchaguzi mkuu ni lugha iliyotumika ya kukebehi ,kukejeli na matusi ikiunganishwa na ushabiki hali iliyoacha makovu na uhasama katika jamii na miongoni mwa viongozi .
Alisema kumekuwa na nyufa katika taifa kwa kuwepo rushwa na ubaguzi kwani rushwa imekuwepo katika ngazi zote za mchakato wa uchaguzi kuanzia uteuzi wa wagombea ndani ya vyama mpaka kutangaza matokeo.
Alisema kumekuwa na ubaguzi wa kila aina ikiwemo ukabila, dini na kikanda ambao nyuma ulijulikana kijiografia lakini sasa zinatumika kisiasa .
Alisema zipo nyufa mpya zinazoanza kujitokeza baina ya wazee na vijana.
Mdahalo huo uliokuwa na kaulimbiu ya ‘Tathmini ya Uchaguzi Mkuu wa Tanzania mwaka 2015: Mchango wa waangalizi wa ndani kuelekea uchaguzi bora, huru na haki’, mgeni rasmi alikuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe.
Mwakyembe alisema takwimu za mwaka 2013-2014 zinaonesha kuwa kwa ujumla demokrasia nchini inazidi kuimarika na kushamiri.
Waziri alisema inaonesha kuwa Tanzania ilikuwa nchi ya 83 ikiwa na alama 50.5 kwa kukidhi vigezo vya demokrasia, ikilinganishwa na Kenya iliyochukua nafasi ya 93 ikiwa na alama 48.1. Zambia ilichukua nafasi ya 94 alama 48.1; Nigeria nafasi ya 107, alama 40.6 na Afrika ya Kusini ikichukua nafasi ya 71 alama 54.7.