MWANASIASA mkongwe nchini, Dk Chrisant Mzindakaya amesema wazee mkoani Rukwa wanaipongeza Serikali ya Rais John Magufuli kwa kuanza vizuri kusimamia nidhamu, uwajibikaji na kudhibiti matumizi yasiyo ya lazima serikalini.
Dk Mzindakaya ambaye ni mwenyekiti wa wazee mkoani humo, alisema kwa sasa kila mwananchi bila kujali itikadi yake ya kisiasa wameridhika na jitihada hizo zinazofanywa na Serikali ya Rais Magufuli.
“Baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani nikizungumza nao wanaeleza waziwazi kuridhishwa kwao na hatua za makusudi zinazochukuliwa na Serikali ya Rais Magufuli ya kurejesha nidhamu na uwajibikaji serikalini. Tumwombee Rais wetu na Serikali yake ili aweze kutimiza yale aliyokusudia kwa maendeleo ya Taifa hili letu,” alisisitiza Dk Mzindakaya.
Mwanasiasa huyo mkongwe alieleza hayo wakati akiwasilisha salamu za wazee wa mkoa wa Rukwa kwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye. Nape alikuwepo mjini hapa kwa ziara ya siku moja. Katika ziara hiyo alikutana na wadau wa wizara yake kutoka mkoani Rukwa katika kikao kilichofanyika mjini Sumbawanga.
Aidha, Dk Mzindakaya alimshangaza Nape baada ya kumkabidhi picha inayomuonesha yeye (Mzindakaya) akiwa baba mzazi wa waziri huyo, Moses Nnauye mwaka 1978.
“Nimeamua leo niku ‘surprise ‘(kushtukiza) nakukabidhi hii picha ambayo nimelazimika kuichukua nyumbani kwangu na kukupatia wewe, nilipiga picha hii na baba yako mzazi (Nnauye),’’ alisema.
|
0 Comments