Watu wasiopungua 34 wameaga dunia nchini Rwanda kufwatia mafuriko makubwa katika maeneo ya kaskazini mwa nchi hiyo.
Kulingana na mwandishi wa BBC nchini humo, barabara inayounganisha mji mkuu Kigali na miji ya Musanze na Rubavu Kaskazini Magharibi mwa Rwanda imekuwa haipitiki.

Vilima vilivyoko eno hilo vimeporomoka na kufunika barabara hiyo.
Hasara iliyopatikana kufwatia mafuriko hayo ni kubwa kwa mujibu wa naibu mkuu wa wilaya ya Gakenke ambayo imeathiriwa sana na mafuriko hayo .
Kiongozi huyo Bi Catherine Uwimana amesema
“Mvua kubwa ilinyesha tangu Jumamosi na kusababisha maporomoko makubwa ya ardhi ambayo hadi sasa watu 34 wamefariki dunia.
''Watu 19 waliojeruhiwa wamelazwa katika hospitali na zahanati za eneo hilo.
''Nyumba zaidi ya 400 zimeharibika kabisa huku miundo mbinu kama madaraja,barabara zinazounganisha kata,waya wa umeme, simu na mkonga wa mawasiliano yaani kila kitu kimesombwa na maji.”
Bi Uwimana ameonya kuwa kuna hofu ya maafa zaidi kwa sababu mvua bado inaendelea kunyesha kwa wingi katika eneo hilo.