Takriban watu 12 hawajulikani walipo hadi sasa, wakihofiwa kufa maji baada ya boti iliyokuwa ikifanya safari kutoka Mbamba Bay nchini Tanzania kwenda Nkhata Bay Malawi kuzama kwenye Ziwa Nyasa.

Duru za usalama zinasema Boti hiyo haijulikani ilipo wala abiria waliokuwemo ndani yake.
Kamanda wa Polisi mkoani Ruvuma, kusini mwa Tanzania, Zuberi Mwombeji amesema haifahamiki ajali hiyo ilitokea aneo gani la Ziwa.
''Usafiri wa kutoka Mbamba Bay mpaka Nkhata Bay huchukua saa tano mpaka sita, walipoona Nkhata Bay hawajafika waliwasiliana na watu wa Mbamba Bay ndipo ilipojulikana kuwa kuna tatizo limetokea'' alieleza Kamanda Mwombeji.
Chanzo cha ajali hiyo kimeelezwa kuwa hali mbaya ya hewa ziwani, hali inayoaminika kuwa ilisababisha Boti hiyo kupigwa dhoruba.
Shughuli za kuisaka Boti iliyotoweka zinaendelea.