Dereva wa basi la mwendo kasi akitoa maelekezo kwa abiria mara baada ya usafiri huo kuanza kwa kishindo juzi.
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ameongeza siku nne zaidi kwa Kampuni ya UDA-RT kutoa elimu ya matumizi ya mabasi yaendayo haraka na wananchi kuendelea kupanda bure hadi Jumatatu watakapolipia.
Akizungumza wakati wa kuangalia mwendelezo wa mafunzo ya matumizi ya mabasi yaendayo haraka, Makonda alisema hatua hiyo imetokana na kufikiwa makubaliano na uongozi wa kampuni hiyo ili kutoa muda zaidi kwa wananchi wengi kupata elimu hiyo.

“Nimeomba siku zaidi ili wananchi wangu wa Dar es Salaam wazidi kupata elimu, hivyo wananchi wataanza kulipa nauli Jumatatu. Tunataka ifikapo Jumatatu kusiwe na mwana- Dar es Salaam atakayelalamika kuwa hajui kutumia tiketi, hajui pa kupandia au kushuka,” alisema.
Makonda alisema katika muda huo wa nyongeza, mabasi yatafanya kazi kuanzia saa 12 asubuhi mpaka saa moja jioni na kuwataka wananchi kutumia fursa hiyo kujifunza zaidi. Aidha, Makonda amewaonya madereva wa bajaji, pikipiki na magari ambayo hayatakiwi kutumia barabara ya mabasi yaendayo haraka kuacha tabia hiyo mara moja, kinyume chake watachukuliwa hatua kali za kisheria.
Alisema kuanzia sasa kumepangwa askari 43 watakaolinda miundombinu ya barabara kuitaka jamii kulinda miundombinu hiyo ambao imetumia fedha za walipakodi. Aliwataka wananchi kuacha tabia ya kugombea kuingia kwenye mabasi na kuzunguka na usafiri huo jambo ambalo linakosesha fursa kwa watu wengine. “Kuna jambo ambalo sio zuri, watu wanapanda mabasi na kuzunguka nayo, sijui hawa watu hawasikii njaa wala kiu.
Hii si nafasi ya kuona basi jipya bali ya kujifunza, ukipanda safari moja shuka na pisha wengine. Pia tujenge tabia ya kupanga foleni na si kugombea kwani sasa kutakuwa na mabasi 80 wakati wa mazoezi,” alisema Makonda ambaye alianza safari yake Kariakoo hadi Kimara Mwisho na kumalizia safari kituo cha Morocco.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa UDA-RT, David Mgwasa alisema watatekeleza agizo hilo na kutumia muda huo kutathmini changamoto zinazojitokeza ili kuzitatua kabla ya kuanza rasmi kutoa huduma hiyo.
Mgwasa alisema kuna mabasi ya aina mbili yale ya haraka (express) yanayotumia vituo vichache na kutumia muda wa dakika 27 hadi 30 na yale ya kawaida yatakayosimama kila kituo na yatatumia kati ya dakika 45 hadi 48.
Manfred Luambano alisema changamoto kubwa ni matumizi mabaya ya vifaa ndani ya gari. “Kuna vifaa ndani ya gari mfano vifaa vinavyotumika kujishikilia mtu asidondoke, lakini watu wamekuwa wakibembea navyo na kupima uzito jambo ambalo limefanya baadhi vikatike,” alisema Luambano.
Daladala 400 zaondoka Daladala 400 zinazotoa huduma ya usafiri katika barabara ya Morogoro, zinatakiwa kuondoka kupisha mradi wa mabasi yaendayo haraka kutokana na kulipwa gharama zote za kuondoka katika barabara hiyo.
Imeelezwa kuwa mabasi mengine yatakayobaki, yatafanya usafiri wa eneo hilo kwa kubadilisha barabara za kupita kutoka barabara ya Morogoro huku tathmini ya hali ya usafiri ikiendelea kufanywa ili kuondoa daladala zote.
Msemaji wa Kampuni ya UDART ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Mkoa wa Dar es Salaam (Darcoboa), Sabri Mabrouk alisema mabasi hayo 400 yatachagua njia watakazotaka kutoa huduma.
Alisema baada ya kufanya tathmini na uhakiki, waliondoa mabasi hayo yaliyokuwa yakifanya huduma ya usafiri katika ruti (njia) 12 za barabara hiyo na yalitakiwa kuondoka katika barabara hiyo kabla ya kuanza kwa mradi.
Alisema kwa sasa kuna daladala 7,500 zinazotoa huduma ya usafiri jijini Dar es Salaam na awamu ya kwanza yote ikimalizika daladala 2,000 zitaondolewa ikiwemo zinazotoa huduma Mwenge, Kawe, Masaki na Kigogo.
Alisema daladala hizo zitaondolewa huku mabasi yaendayo haraka yatakuwa yameingia yasiyopungua 400 lakini kwa sasa kuna mabasi yaendayo haraka 140. Alisema daladala zitakazobaki zitabadilishiwa njia kuanzia wiki ijayo na hazitapita tena barabara ya Morogoro na kutoa mfano ya zinazotoka Mabibo kwenda Kariakoo, zitatumia barabara ya Kawawa ;na zile za Makumbusho Kariakoo na Muhimbili – Kariakoo, zitatumia barabara ya Ali Hassan Mwinyi kupitia Daraja la Selander.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA), Gillian Ngewe alisema vikao vinaendelea kuangalia namna ya kuondoa magari zaidi katika barabara hiyo baada ya kufanya tathmini.
Alisema ni kweli wapo waliolipwa na wanatakiwa kuondoka lakini wataondoka pole pole wakati mamlaka hiyo inaangalia jinsi usafiri huo unavyotoa huduma ili isijekutokea mrundikano wa watu.
Alisema licha ya kuondoa mabasi hayo katika barabara ya Morogoro lakini mahitaji ya daladala bado ni makubwa kwa baadhi ya njia hususan Kigamboni na Chanika ambako yatapelekwa magari yatakayoondolewa huko.
Daladala zalia Kuanza kwa huduma hiyo kumeathiri biashara ya wenye mabasi ya abiria ya daladala baada ya kujikuta wakiwa na abiria wachache waliotosha viti ikiwa ni tofauti na siku za nyuma ambapo watu walikuwa wanajaa.
“Tangu kuanza mabasi ya haraka najikuta naenda safari moja kwa kupata chini ya 10,000, hii ni tofauti na awali,” alisema Rashid Juma na kuongeza kuwa wanaopanda ni wale wasiotaka kupanda bure.
Naye John Michael anayefanya kazi safari za Simu2000 -Kariakoo alisema amelazimika kupaki gari nyakati za mchana tangu kuanza huduma hiyo. “Kuanzia saa nne abiria wanapungua kiasi, kutokana mabasi ya haraka tumelazimika kupaki na kusubiri nyakati za asubuhi na jioni ili tuweze kuambulia abiria,” alisema.
“Sisi tunaotoka pembezoni mwa barabara kuu, tunashukuru Mungu tunapata abiria ingawa wale wa njiani wamepungua,” alisema konda Khalifan Kondo anayefanya safari zake Makumbusho-Sinza-Posta.
Habari hii imeandikwa na Anastazia Anyimike na Theopista Nsanzugwanko.