Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongela.
WATU saba wa familia moja wameuawa kikatili wilayani Sengerema mkoani Mwanza juzi usiku. Taarifa iliyotolewa na Ofisa Habari wa Mkoa wa Mwanza, Atley Kuni ambaye alifuatana na Mkuu wa Mkoa huo, John Mongella na Kamanda wa Polisi Mkoa, Ahmed Msangi katika eneo la tukio, alisema watuhumiwa katika tukio hilo hawajajulikana.

Kuni aliwataja waliopoteza maisha katika tukio hilo kuwa ni Augenia Philipo (62), Maria Philipo (56), Yohana Mabula (20), Regina Aloyce (12) na Mkiwa Philipo (13) huku wengine wawili wakitambulika kwa jina moja kila mmoja kuwa ni Donald na Samson.
Aidha, chanzo cha mauaji hayo ya kikatili hakijajulikana, ingawa Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Zainab Telack alisema huenda mauaji hayo inawezekana yakawa ni ya kulipiza kisasi. Vyanzo vingine vinaarifu kuwa mauaji ya namna hiyo ni ya kawaida katika maeneo hayo, hasa msimu huu ambao kaya nyingi zinakaribia msimu wa mavuno.
“Bado kuna mkanganyiko juu ya chanzo cha mauaji hayo, wapo wanaosema kuwa huenda ni ya kulipiza kisasi lakini pia wengine wanasema yanatokana na msimu wa mavuno, lakini tunaamini uchunguzi wa Polisi ndio utakuja na majibu sahihi na ambao umeshaanza kazi hivi tunavyoongea,” alisema Kuni.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mongella alipopigiwa simu na gazeti hili jana saa 10 jioni, alieleza kuwa yuko katika kikao na akaomba apigiwe baada ya saa mbili, wakati Kamanda wa Polisi Mkoa, Msangi hakupatikana mara moja kuzungumzia suala hilo. Hata hivyo, taarifa za awali zilisema kuwa Mkuu wa Mkoa ametoa saa 48 kwa vyombo vya dola kukamata wauaji hao na kuwafikisha mbele ya sheria.