|
UMILIKI wa Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA) kwa Jiji la Dar es Salaam, umekoma rasmi baada ya Kampuni ya Simon Group kukamilisha malipo ya ununuzi wa hisa za jiji hilo katika shirika hilo ambazo ni asilimia 51.
Kutokana na kukamilika kwa malipo hayo, sasa Uda inamilikiwa Kampuni ya Simon Group yenye asilimia 51 ya hisa ambazo ndizo zilizokuwa hisa za Jiji na Serikali yenye asilimia 49. Akizungumza Dar es Salaam jana, Msajili wa Hazina, Lawrance Mafuru alisema mpaka katikati ya Aprili, mwaka huu, Kampuni ya Simon Group ilikuwa imemaliza kulipia malipo ya hisa zote zilizokuwa zikimilikiwa na Jiji.
Kwa mujibu wa Mafuru, sasa Serikali inapaswa kuitambua Kampuni ya Simon Group kuwa mwenye hisa katika shirika hilo, kwa kuwa kampuni hiyo imewasilisha nyaraka za ununuzi wa hisa hizo na Jiji limethibitisha kupokea fedha zao na kukubali kwamba muamala huo wa malipo ni halali.
Akifafanua namna ununuzi huo ulivyo halali, Mafuru alisema Jiji walifungua kesi kuomba mahakama iagize Kampuni ya Simon Group ilipe fedha za hisa za Jiji kufikia Aprili 30 mwaka huu, kinyume cha hapo hisa hizo zirudishwe kwa Jiji la Dar es Salaam.
Kwa maelezo hayo ya Mafuru, kwa kuwa Kampuni ya Simon Group wamefanya hivyo kama walivyotakiwa na Mahakama, sasa ndio wamiliki halali wa asilimia 51 ya hisa za UDA na kama wangeshindwa, hisa hizo zingerudi kwa Jiji la Dar es Salaam.
Hata hivyo, alisema katika kuhakikisha uhamishaji huo wa hisa unakuwa halali, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imeanza kudai kodi ya malipo hayo ya ununuzi wa hisa kutoka kwa jiji, ndio jina la umiliki libadilishwe kwa Msajili wa Makampuni (BRELA).
Alisema Serikali sasa inashiriki kupitia vitabu vya UDA, ili kuhakikisha vinaendeshwa kwa kufuata utawala bora kama ilivyo katika kampuni zingine ya Serikali. Mafuru alisema kama ilivyoagizwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), sasa Serikali itashiriki kusimamia mabasi yaendayo haraka jijini Dar es Salaam na kazi ya kwanza ni kuondoa makandokando yote yaliyokuwepo na kusimamia uendeshaji wake.
Alisema mgogoro wa umiliki wa UDA, ulisababishwa na Bodi ya shirika hilo, kutaka kuuza hisa za Serikali ambazo ni asilimia 49 wakati haina mamlaka ya kisheria ya kufanya hivyo.
Alifafanua kwamba, uamuzi wa kuuza hisa za Serikali ni wa Baraza la Mawaziri pekee na kwa kuwa hakuna kikao cha aina hiyo kilichowahi kufanya uamuzi huo, Bodi hiyo ilifanya makosa kutaka kuuza hisa hizo, jambo lililodhihirisha kuwepo masuala ya ubadhirifu na rushwa.
0 Comments