WIKI moja baada ya Serikali kutangaza kuanzishwa kwa Divisheni ya Mahakama ya Rushwa na Ufisadi katika Mahakama Kuu, Rais John Magufuli amewaibukia mawakili wa Serikali, akiwatuhumu kwa kushirikiana na mawakili wa wahalifu ili Serikali ishindwe kesi. Aidha amewaonya polisi kwa kuingia mikataba inayotia mashaka baina yao na wawekezaji.

Mahakama ya ufisadi inatarajiwa kutumika kushughulikia watuhumiwa wa rushwa na ufisadi, wakiwemo waliokwisha tumbuliwa, lakini kesi zake zinatarajiwa kuanza kunguruma Julai mwaka huu.
Akizungumza mkoani Dodoma jana wakati akifungua kikao kazi cha makamanda wa polisi wa mikoa, mawakili wafawidhi wa Serikali wa mikoa na wakuu wa upelelezi wa mikoa na vikosi, Rais Magufuli alisema mawakili hao wakiona kesi inayohusu fedha imeingia, wanasema ‘dili’ limeingia.
“Kumekuwa na usemi kwa baadhi ya wapelelezi na mawakili wachache, nasema wachache... Panapokuwa na kesi inayohusu fedha, wana misemo yao wanasema dili limepatikana.
“Saa nyingine kesi inapopelekwa mahakamani wanashirikiana na mawakili wa Serikali na mawakili wanaomtetea mhalifu na wanaposhirikiana siku zote Serikali inashindwa,” alisema.
Alionya kuwa hali hiyo inapoonekana kila siku Serikali inashindwa katika kesi, kunakuwa na kigugumizi cha kuwezesha mawakili hao pale wanapopeleka maombi. “Niwaombe mawakili na polisi wanaohusika na upelelezi mtangulize maslahi ya nchi mbele,” alisema na kuongeza kuwa amekuwa akisikitishwa na vitendo vya Serikali kushindwa katika kesi nyingi mahakamani licha ya kuwa na wanasheria mahiri.
Ulaji wapelelezi Awali kabla ya kutoa hotuba yake, Rais Magufuli aliwapa nafasi makamanda na mawakili wafawidhi hao kutoa maoni yao juu ya changamoto zinazowakabili katika kutekeleza wajibu wa kufanya upelelezi na kuendesha mashitaka.
Katika maoni yao, watendaji hao wanaohusika zaidi katika kupeleleza na kushitaki watuhumiwa mahakamani, walidai ufinyu wa bajeti ndio sababu kubwa ya kucheleweshwa kwa kesi hizo.
Akizungumzia changamoto hiyo, Rais Magufuli aliahidi kuwatafutia fedha watendaji hao kwa ajili ya kukabiliana na changamoto hizo, lakini akawataka fedha zitakazotafutwa zitumike vizuri.
Mikataba ya hovyo Akisisitiza umuhimu wa fedha hizo kutumika vizuri, Rais Magufuli alisema kuna taarifa zinaonesha Jeshi la Polisi, limekuwa likihusishwa na matumizi mabaya ya fedha hali inayoongeza ukubwa wa matatizo yanayokwamisha utendaji wake wa kazi.
Alitoa mfano wa taarifa za matumizi mabaya ya fedha zinazotolewa kwa ajili ya kununua vifaa na sare za askari, ama mikataba yenye mashaka inayotiwa saini kati ya polisi na wawekezaji kuwa ni baadhi ya mambo yanayoongeza hali ngumu ya utendaji kazi kwa jeshi hilo.
“Oysterbay pale ni eneo ambalo ni zuri sana, kila mmoja anajua, mmeingia kwenye mikataba mnayoijua nyinyi, mkapewa mtu anawajengea pale, sifahamu kama majengo hayo yanafaa.
“Palikuwa na ubaya gani eneo la Oysterbay likawa na hati, mkaitumia hiyo hati kwenda kukopa benki na kujenga nyumba hata za ghorofa 20 pale, mkaweka kitegauchumi na polisi wenu wakakaa pale?
“Nimesema lazima nizungumze kwa uwazi, nisiposema kwa uwazi nitajisikia vibaya nikimaliza mkutano huu. Nataka muelewe na muelewe ukweli mwelekeo ninaoutaka mimi,” alisema Rais Magufuli.
Alisisitiza kwa Jeshi la Polisi kujiepusha na kashfa ambazo zimekuwa zikisemwa dhidi yake, ikiwemo maofisa wa Polisi kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya na kuazimisha silaha kwa wahalifu wa ujambazi.
Hata hivyo, Rais Magufuli alilipongeza jeshi hilo na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka kwa kazi kubwa wanayoifanya na ametaka apelekewe mpango wa mahitaji yao ili atafute namna ya kuimarisha vyombo hivyo.