RAIS John Magufuli amesema nafuu ya shetani kuliko watumishi hewa na kubainisha kuwa mpaka juzi, imebainika kuwapo kwa watumishi hewa 10,295 serikalini.
Amesema kati yao watumishi hao, 8,373 wanatokea Tawala za Mikoa na Seriali za Mitaa (Tamisemi) na 1,922 wanatoka Serikali Kuu.

Akihutubia Taifa jana katika Siku ya Wafanyakazi Dunia kitaifa kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma, Rais Magufuli alisema watumishi hewa hao wamekuwa wakilipwa fedha nyingi ambazo zingeweza kurekebisha maslahi ya wafanyakazi halali na kutekeleza miradi ya maendeleo.
Alisema watumishi hewa walikuwa wakilipwa kila mwezi zaidi ya Sh 11,603,273,799.41 na kwa mwaka wamelipwa kwa zaidi ya Sh 139,239,239,285.92 na ukizidisha malipo hayo kwa miaka mitano utapata Sh 696,196,427,964.06 ambazo zililipwa kwa watumishi hao hewa.
“Ukizidisha miaka mitano ya kuwa na wafanyakazi hewa, utapata kuona kuwa wamelipwa zaidi shilingi 696,196,427,964.06. Kwa miaka mitano, hizi bilioni 696 zingetosha kujenga madaraja matatu kama lile Daraja la Nyerere la Kigamboni, Flyover zinazojengwa Dar es Salaam zinazojengwa kwa msaada na mkopo kutoka Japan zingekuwa saba,” alifafanua Dk Magufuli.
Alihoji fedha hizo Sh bilioni 696 kama zingetumika kulipa mishahara ya wafanyakazi halali, wafanyakazi wangeongezewa mshahara kiasi gani, na endapo pia zingetumika kujenga hospitali zingejengwa ngapi, barabara, shule na kununua dawa.
Aidha, alisema mbaya wa wafanyakazi ni mfanyakazi mwenyewe, hivyo anawaomba wananchi kuunga mkono juhudi za serikali za kuwafukuza na kufichua watumishi hewa.
“Ni nafuu ya shetani kuliko watu hawa… hawajali shida za watu wengine, hawajali maslahi ya wengine, wewe unahangaika wao wanaishi maisha ya ajabu, ndio maana nataka hao nilale nao mbele naomba mnisapoti. Najua bado wapo na wako kwenye maeneo yote,” aliongeza Rais Magufuli.
Alitoa mfano wa mtu anapoajiri anakuwa na wafanyakazi hewa 20 hadi 30 mishahara yote anachukua yeye na kugusia suala la mfanyakazi mmoja wa Mamlaka ya Mapato (TRA) aliyekuwa anapokea mishahara 17.
Alisema wapo watu waliolipwa mishahara ambao wamefungwa, wamekufa na hata waliostaafu.
“Hiyo ndio Tanzania tuliyokuwa tumefikia, wachache wasio waaminifu ni wabaya kuliko shetani hawajali shida za watu wengine hawajali mateso ya wafanyakazi wengine, wewe unalia hela haitoshi unatakiwa kulipa pango, umeme maji, mtoto anaumwa, yunifomu wao wanaishi maisha ya ajabu. Nataka nilale nao mbele naomba mnisapoti,” alieleza Rais Magufuli.
Alisema serikali imekuwa ikilipa Sh bilioni 573 kwa ajili ya kulipa mishahara na mingine ni mishahara hewa kwenye hifadhi za jamii, fedha kwa ajili ya matibabu, likizo, likizo za uzazi, matibabu na kuna madai hewa.
“Tupo hapa tulipo tufanye kazi mahewa yote tuyafukuze ili Watanzania waweze kufaidi, inasikitisha sana wakati mwingine najiuliza kwa nini niliomba Urais najitahidi kutafuta fedha kwa ajili ya mishahara, kutekeleza fedha za serikali ya elimu bure, kutafuta fedha kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu lakini unakuta mtu anapanga mikakati ya kulipa malipo hewa,” alisema Dk Magufuli.
Aliwataka watumishi legelege, wabadhirifu na wala rushwa kubadilika kutokana na vitendo hivyo, lakini aliwapa moyo watumishi wote waadilifu na wachapa kazi na kuwataka kuendelea kufanya kazi na yeye yupo pamoja nao huku akiwataka kuwapuuza wale wote ambao wamekuwa wakiwabeza wafanyakazi.
“Napenda pia kutumia fursa hii kuwatia moyo wafanyakazi ambao ni wachapa kazi na ambao wanatekeleza majukumu yao kwa weledi na uaminifu, endeleeni kufanya kazi kwa kujiamini, kujituma bila kuwa na wasiwasi wowote mimi nipo pamoja na ninyi,” alisema Magufuli.
Alisema wapo baadhi ya watu wanaowatisha na kuwaeleza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano haijali wafanyakazi na kuwataka kuwapuuza watu hao kwani hao ndio wale waliokuwa wakinufaika na kushirikiana na watumishi mafisadi, wala rushwa na wabadhirifu.
“Mkitoka leo hapa ukamsikia mfanyakazi yeyote anakuambia Serikali ya Awamu ya Tano haiwapendi wafanyakazi ujue yule ni miongoni mwao mwa wale waliokuwa wanafaidika na ujue hao wanatapatapa baada ya kuona serikali inachukua hatua mahususi kwa watumishi wa namna hiyo,” alisema Magufuli.
Alisema Serikali ya Awamu ya Tano haitambagua mfanyakazi yeyote ambaye anajituma na kufanya kazi kwa weledi na uaminifu na kuahidi kuwa serikali yake itaendelea kuwatetea na kuwalinda wafanyakazi waadilifu.
Alisema si kweli kuwa serikali yake haiwataki wafanyakazi, na kufurahishwa na hatua ya Tucta ya kuunga mkono hatua ya serikali ya kuwachukulia hatua watumishi wasio waaminifu kwa staili maarufu kama kutumbua majipu.
Katika risala yao ya Tucta iliyosomwa na Katibu Mkuu, Nicholaus Mgaya, walimpongeza Rais Magufuli kutokana na jinsi serikali yake ilivyoleta matumaini kwa wafanyakazi na tofauti imeonekana na serikali zilizopita kwani hapo awali usimamizi wa sheria zilizopo haukuwa wa dhati na kijasiri kama ilivyo sasa.
“Lakini baada ya Serikali yako kuingia madarakani tumeshuhudia usimamizi wa utawala wa kisheria ukifanyika kwa dhati na kwa ujasiri hadi kuanza kurudisha matumaini ya wafanyakazi ambayo yalikwishaanza kupotea. Tunaamini kwamba dhana ya mabadiliko uliyoingia nayo madarakani italeta ufanisi, maendeleo na kuondoa rushwa na ufisadi aidha itagusa utawala wa sheria ambao ni pamoja na usimamizi thabiti wa sheria za kazi ili kuondoa kabisa kero za wafanyakazi zitokanazo na usimamizi dhaifu wa sheria hizi. “Tunaamini Serikali ya Awamu ya Tano itajenga mfumo imara na thabiti wa kitaasisi utakaodumu ili mapambano dhidi ya ufisadi yawe endelevu,” alisema Mgaya.