|
SERIKALI ya Awamu ya Tano imeanza kutekeleza kwa vitendo azma yake ya kujenga uchumi unaotegemea viwanda baada ya kuzindua ujenzi wa mradi maalumu wa uwekezaji wa viwanda mkoani Morogoro ili kukuza uchumi na kuongeza ajira nyingi kwa vijana nchini.
Utekelezaji huo ni kutokana na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Charles Mwijage juzi kuzindua eneo maalumu la ujenzi wa miradi ya uwekezaji la Star City katika Manispaa ya Morogoro.
Eneo hilo la miradi ya uwekezaji lina ukubwa wa ekari 10,661 na lilikuwa ni shamba la mkonge Tungi Sisal Estate ambalo kwa sasa likijulikana kwa jina la Dominio Plantation Limited (DPL).
Waziri Mwijage kabla ya kuzindua eneo hilo maalumu la uwekezaji, alisema Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli imeanza utekelezaji wa Tanzania kuwa nchi ya viwanda kwa kuanza na Mkoa wa Morogoro.
“Morogoro haijapendelewa isipokuwa ina historia tangu wakati wa Serikali ya Awamu ya Kwanza ya Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere ambapo Waziri Jamal (Amir) aliwezesha kujengwa kwa viwanda hivi hapa Morogoro,” alieleza Mwijage na kuongeza: “Morogoro ina bahati ya kuwa na sifa ya kujenga viwanda kutokana na mazingira na jiografia yake naweza kusema ina bahati ya kuzaliwa ilivyoumbwa na Mungu kuvutia uwekezaji.”
Alisema ujenzi wa viwanda katika maeneo mbalimbali yaliyotengwa ya uwekezaji ni mpango wa Serikali ya Awamu ya Tano ya kuona vinawatoa vijana kwenye kucheza ‘pool’, bao na kukaa vijiweni ili wajikite katika shughuli halali za uzalishaji mali viwandani ili kujipatia kipato na kukuza uchumi wa taifa.
Alisema kutokana na kutengwa kwa eneo hilo maalumu la uwekezaji, tayari Kampuni ya Kutengeneza nguo za michezo ya Mazava imesaini makubaliano na Dominio Plantation Limited (DPL) ili kupatiwa eneo kubwa la kujenga kiwanda cha kisasa kitakachokuwa na uwezo wa kuajiri vijana zaidi ya 7,000.
“Katika ujenzi wa awamu ya kwanza ya uendelezaji eneo hili utaanza kwa kujengwa kwa viwanda vikubwa kikiwemo cha Mazava ambacho kitatoa ajira kwa watu zaidi ya 7,000 na viwanda vingine pia kujengwa,” alisema.
Pia alisema eneo hilo litakuwa na viwanda vidogo vidogo, maduka makubwa, eneo la ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa pamoja na Bandari Kavu itakayosaidia kuondoa msongamano wa mizigo Bandari ya Dar es Salaam.
Kutokana na uwekezaji huo na serikali kuendelea kutenga maeneo maalumu ya uwekezaji katika mikoa mbalimbali, Waziri Mwijage aliitaka Mamlaka ya Elimu na Ufundi Stadi (VETA) ijiandae kikamilifu kwa ajili ya kutoa mafunzo ya ufundi kwa vijana watakaoweza kufanya kazi katika viwanda.
“Tusisubiri viwanda vijengwe halafu tuanze kuhangaika kuwapata vijana wenye ujuzi wa kufanya kazi mbalimbali za viwandani…hili ni jukumu la Veta kuona vijana wanapatiwa ujuzi utakaowawezesha kuingia katika soko la ajira za viwanda,” alieleza Mwijage.
Pamoja na hayo, walitumia fursa hiyo kuzitaka halmashauri za wilaya, manispaa, majiji kutenga maeneo ya ardhi ngazi ya kata yatakayotumiwa na vijana kuanzisha viwanda vidogo vidogo vitakavyoongeza kutoa ajira.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Kebwe Steven alipongeza kuanzishwa kwa eneo hilo maalumu la uwekezaji na kutoa ekari 600 kati ya hizo 500 za kujenga bandari kavu na ekari 100 kwa ajili ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji Tanzania (EPZA), Joseph Simbakalia alisema wataendelea kutoa mchango wa kuendeleza viwanda mkoani Morogoro.
0 Comments