Kesi dhidi ya mwanamke mfanyabiashara raia wa China anayetuhumiwa na mashtaka ya kuendeleza mtandaoa wa kihalifu wa ulanguzi wa pembe barani Asia imeahirishwa kwa wiki mbili nchini Tanzania.
Alifikishwa mahakamani Jumatatu asubuhi mjini Dar es Salaam.

Waendesha mashtaka wanasema Yang Feng Glan, anayejulikana kwa umaarufu pia kama Malkia wa pembe, aliendesha biashara haramu ya kuwaua ndovu katika mbuga za wanyama ili kupata pembe zao ambazo wanazisafirisha na kuziuza katika mataifa ya bara Asia.
Anashutumiwa kwa kuendeleza shughuli hiyo kwa takriban miaka 14.
Anakana mashtaka hayo.
Mahakama imeambiwa kwamba faili ya kesi yake bado imo mikononi mwa mkurugenzi wa mashtaka ya umma.
Maafisa wa serikali Tanzania walitaja kukamatwa kwa Yang Feng Glan mnamo Oktoba mwaka jana kama ufanisi mkubwa.
Taifa hilo la Afrika mashariki limepoteza thuluthi mbili za ndovu wake katika kipindi cha miaka kumi iliyopita.