WATUHUMIWA sita kati ya 11 wa udhalilishaji, ubakaji na usambazaji wa picha za video, zikimwonesha msichana mwenye umri wa miaka 21, akilazimishwa kufanya mapenzi eneo la Dakawa, Morogoro wamepandishwa kizimbani. Imebainika kuwa miongoni mwa makosa yanayowakabili, lipo pia la kulawiti.

Mamia ya wakazi wa Manispaa ya Morogoro walifurika katika jana katika viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Morogoro, kushuhudia watuhumiwa hao wakipandishwa kizimbani. Watuhumiwa hao walifikishwa mahakamani hapo na walisomewa mashitaka yao na mahakimu wawili tofauti katika vyumba vya mahakama hiyo.
Wawili katika watuhumiwa hao, wanakabiliwa na shitaka la kubaka , kulawiti na kupiga picha za video za kujamiiana na kuzisambaza kwenye mitandao ya kijamii. Walioshitakiwa kwa kosa kumlawiti na kumbaka msichana huyo kisha kupiga picha za video wakati wakifanya tendo la kujamiiana kwa lengo la kuzisambaza picha hizo kwenye mitandao ya kijamii, ni Idd Adamu (32) mkazi wa Makambako, mkoani Iringa na Zuberi Thabiti (30) mkazi wa Mbalali, mkoani Mbeya.
Ulinzi katika viwanja vya mahakama hiyo, uliimarishwa huku wananchi na waandishi wa habari, wakizuiwa kuingia kusikiliza kesi hiyo ikisomwa ndani ya mahakama. Hali hiyo ilielezwa na uongozi wa mahakama kuwa inatokana na matakwa ya sheria ya makosa ya ubakaji na ulawiti, kuzuia kesi hiyo kusomwa hadharani.
Watu walijaa kila kona na ilielezwa kuwa kesi hiyo ni ya aina yake, kutokana na kugusa hisia za wengi. Baadhi ya watu nje ya mahakama, walionekana wakilia na miongoni mwao walidai wanamuonea huruma msichana aliyetendewa unyama huo, kwani baadhi ya wahusika waliosambaza picha hizo mitandaoni, wana undugu na msichana huyo.
Akisoma shtaka linalowakabiliwa watuhumiwa wawili wa makosa ya ubakaji, ulawiti na kupiga picha za video wakati wakifanya tendo la kujamiiana kwa lengo la kuzisambaza picha hizo kwenye mitandao ya kijamii, Wakili wa Serikali, Gloria Rwakibalila mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mkoa, Mary Moyo, alidai kuwa washtakiwa hao kwa pamoja walitenda kosa hilo Aprili 27, mwaka huu.
Alidai watuhumiwa walitenda kosa hilo Aprili 27 , mwaka huu majira ya jioni katika nyumba ya kulala wageni iliyofahamika kwa jina la Titii iliyopo Dakawa wilayani Mvomero. Aidha, watuhumiwa hao wawili waliunganishwa na watuhumiwa wengine wanne waliofikishwa mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Ivan Msack kwa kosa la kusambaza picha za video za kujamiiana kwenye mitandao ya kijamii, ikiwamo ‘WhatsApp’, jambo ambalo ni kosa chini ya Sheria ya Makosa ya Mitandao ya mwaka 2015 Kifungu Namba 14 (1b) na (2b).
Washtakiwa hao ni Rajabu Salehe (30), Ramadhan Ally (26), Musini Ngai (36) na John Peter (26), wote wakiwa ni wakazi wa Dakawa Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro. Alidi kuwa washitakiwa hao wote kwa pamoja, walitenda kosa hilo katika nyakati tofauti kati ya Aprili 28 hadi 30, mwaka huu, ambapo walisambaza picha hizo huku wakijua kufanya hivyo ni kosa kisheria.
Baada ya kusomewa mashtaka yao, ambapo wote walikana, upande wa mashtaka ukiongozwa na Wakili wa Serikali, Gloria Rwakibalila, Edga Bantulaki na Calstus Kapinga, uliwasilisha mahakamani hapo hati ya zuio la dhamana kwa washtakiwa hao.
Katika hati hiyo, upande wa mashtaka ulidai kuwa endapo washtakiwa hao watakuwa nje kwa dhamana, wataharibu upelelezi wa kesi hiyo na pia kutahatarisha usalama wa mlalamikaji na washtakiwa hao, kutokana na kesi hiyo kuvuta hisia za watu wengi.
Mahakama iliahirisha kesi hiyo hadi Juni Mosi mwaka huu, itakapotajwa tena na kusikiliza suala la dhamana, kufuatia maamuzi ya maombi hayo ya pande mbili. Washitakiwa wote sita walirudishwa rumande.
Wakati kesi ikiendelea mahakamani hapo baadhi ya watu waliokuwemo waliangua kilio huku baadhi yao walisikika wakidai kuwa baadhi ya washitakiwa waliosambaza picha wanauhusiano wa kindugu na binti huyo.
Katika hatua nyingine, kabla ya kufikishwa watuhumiwa hao mahakamani, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei alikutana na waandishi wa habari na alisema kuwa kati ya watuhumiwa 11 waliokuwa wamekamatwa, sita upelelezi wake ulikamilika. Alisema watuhumiwa wengine watano, upelelezi unaendelea na ukikamilika watafikishwa mahakamani.