Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) anayeshughulikia Utumishi na Utawala Bora, Selemani Jafo
UFUNGAJI wa vifaa vya kielektroniki katika hospitali za Serikali katika mikoa mbalimbali, umeibua fukuto la ufisadi mkubwa, uliokuwa ukifanywa katika makusanyo ya fedha wanazolipa wagonjwa kwa ajili ya huduma.
Akizungumza bungeni mjini hapa jana katika kipindi cha maswali na majibu, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo, alisema tangu mfumo huo wa kielektroniki uanze kutumika katika hospitali nyingi nchini, mapato yameongezeka.

Jafo alisema mafanikio hayo ya ukusanyaji wa mapato kwa mfumo wa elektroniki, yamesababisha katika sekta ya afya kwa sasa ajenda kuu iwe kuongezea mapato ya hospitali zote nchini, kuendane na utoaji wa huduma bora.
Hospitali ya Rufaa Mbeya Akitoa mfano wa Hospitali ya Rufaa ya Mbeya, Jafo alisema kabla ya kufungwa kwa vifaa hivyo, ilikuwa ikikusanya Sh milioni 70 kwa mwezi, lakini baada ya kufungwa vifaa hivyo, mapato yameongezeka zaidi ya mara saba na kufikia Sh milioni 500 kwa mwezi.
Taarifa zinaonesha pamoja na ongezeko hilo la mapato, bado hospitali hiyo iliendelea kukosa vifaa muhimu vya tiba, ikiwemo mashine ya CT-Scan, kiasi cha kusababisha mwanzoni mwa mwaka huu Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Hamis Kigwangalla kuwajia juu watendaji wake.
Dk Kigwangalla alielezea kushangazwa kuona hospitali hiyo ikikusanya Sh milioni 500 kwa mwezi, huku ikidai kukosa CT-Scan na kutoa siku 60 kifaa hicho kifungwe. Katika maelezo aliyopewa, Dk Kigwangalla alielezwa kuwa ingawa ni kweli hospitali hiyo inakusanya Sh milioni 500 kwa mwezi, lakini mahitaji ya dawa pekee yanachukua zaidi ya Sh milioni 300, kabla ya gharama nyingine ikiwemo za usafiri wa magari.
Alielezwa kuwa hospitali hiyo imejipanga kuchukua mkopo kutoka Mfuko wa Bima ya Afya ya Taifa (NHIF), kwa kuwa ili kupata mashine hiyo, wanapaswa kuwa na kuanzia Sh milioni 800 mpaka Sh bilioni 1.2.
Sekou Toure Mbali na Mbeya, katika Hospitali ya Mkoa wa Mwanza ya Sekou Toure kwa mujibu wa Jafo, kabla ya kufungwa kwa vifaa hivyo, ilikuwa ikikusanya kati ya Sh 150,000 mpaka 200,000 tu kwa siku.
Jafo alisema baada ya kufungwa vifaa hivyo, mapato hayo yaliongezeka mpaka karibu mara 21 na kufikia Sh milioni 3.2 kwa kila siku. Hospitali ya Tumbi Mbali na Mwanza, Naibu Waziri huyo wa Tamisemi, alisema mkoani Pwani katika Hospitali ya Tumbi, nako kabla kufungwa vifaa hivyo, makusanyo yalikuwa Sh 200,000 kwa siku lakini baada ya kufungwa, mapato yakaongezeka mara 20 na kufikia Sh milioni nne kwa siku.
Kutokana na mafanikio ya hospitali hizo, Jafo aliwataka wabunge wote kufuatilia kwa makini hospitali katika halmashauri zao za wilaya, ili kila moja iweke mfumo wa kielektroniki kwa ajili ya kukusanya mapato katika huduma ya afya.
Aliwataka wabunge hao kuweka kipaumbele katika kuhakikisha hospitali zote katika maeneo yao, zinafungwa mifumo hiyo ya kielektroniki, ili fedha zikusanywe kusaidia katika kuboresha huduma za afya katika maeneo hayo.
“Tusipozingatia haya, hata tukipeleka fedha bado tutakuwa na matatizo, ndio maana ajenda yetu kuu ni kutumia mifumo ya kielektroniki, ili kuongeza mapato katika sekta ya afya,” alisisitiza.
Awali Mbunge wa Mafinga Mjini, Cosato Chumi (CCM), alitaka kufahamu kama Serikali haioni umuhimu wa kuiongezea fedha Hospitali ya Mji wa Mafinga, ili ihudumie kwa ufanisi idadi kubwa ya wagonjwa wanaohudhuria hospitali hiyo.
Pia Mbunge huyo alitaka kufahamu kama Serikali iko tayari kuiongezea hospitali hiyo watumishi mara mbili zaidi ya kiwango inachopata, ili iwe na uwezo wa kutosha kukabiliana na mzigo wa kazi.
Akijibu maswali ya mbunge huyo, Jafo alisema Serikali imekuwa ikiipatia Hospitali ya Mji wa Mafinga Sh milioni 90 kwa ajili ya maendeleo na Sh milioni 90 kwa matumizi mengineyo ; na kwamba inaweza kuongezewa fedha hizo kulingana na wigo wa upatikanaji wa fedha.
Kuhusu watumishi, alisema hospitali hiyo ina watumishi 209 na upungufu uliopo ni wa watumishi 95, sawa na asilimia 31.3 na kwa mwaka wa fedha 2016/17 imeidhinishiwa kuajiri watumishi 18.