RAIS John Magufuli ameiagiza Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi na vyombo vya dola kuchukua hatua mara moja dhidi ya dosari za ukaguzi zilizopo katika kitengo cha ukaguzi wa mizigo na abiria katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (Terminal One) jijini Dar es Salaam.

Taarifa iliyotolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, Ikulu, Gerson Msigwa ilisema Rais Magufuli alitoa agizo hilo jana, alipofanya ziara ya kushtukiza katika uwanja huo na kubaini kuwa mashine za ukaguzi za sehemu ya kuwasili abiria na mizigo, hazifanyi kazi kwa muda mrefu.
Maofisa wa uwanja huo waliokuwa wakitoa maelezo juu ya hali ya kitengo cha ukaguzi wa mizigo na abiria katika uwanja huo, walikuwa wakitoa taarifa zinazotofautiana kuhusu utendaji kazi wa mashine za ukaguzi, hali iliyosababisha Rais Magufuli aamue kuiagiza wizara husika kwa kushirikiana na vyombo vya dola, kuchukua hatua mara moja.
“Unajua mimi sipendi kudanganywa, ni vizuri uzungumze ukweli tu, kwa nini nimeanzia hapa huwezi ukajiuliza? Eeeh sasa sipendi kudanganywa, ukinidanganya nitachukia sasa hivi, wewe umenidanganya kwamba hiyo ndio mbovu na hii ndio nzima, nikawaambia muiwashe hiyo nzima, akaja huyu mwenzako amezungumza ukweli kabisa, akasema hii ni mbovu kwa miezi miwili.
“Kwa hiyo mizigo inayoingia humu huwa hamuikagui kwa namna yoyote ile, kwa hiyo mtu nikiamua kuja na madawa yangu ya kulevya, nikaja na dhahabu zangu, na almasi zangu na meno ya tembo kwa kutumia hizi ndege ndogondogo napita tu,” alisema Rais Magufuli kwa maofisa hao wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere.
Rais Magufuli alifanya ziara hiyo ya kushtukiza baada ya kuwasili katika uwanja huo akitokea jijini Kampala nchini Uganda, ambako juzi alihudhuria sherehe ya kuapishwa kwa Rais wa Uganda, Yoweri Museveni.