MUFTI wa Tanzania, Shehe Abubakar Zuberi.
MUFTI wa Tanzania, Shehe Abubakar Zuberi, amewataka viongozi wa dini ya Kiislamu kumuombea Rais John Magufuli aweze kuongoza nchi kwa misingi ya haki na kutunza rasilimali ziwanufaishe Watanzania wote. Aidha, amewataka kuacha kufanya kazi kwa mazoea na badala yake wawajibike kwa tija na kuleta matokeo chanya.

Mufti alitoa kauli hiyo Dar es Salaam wakati akifungua semina elekezi ya viongozi wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), iliyohusisha mashehe wa mikoa, wenyeviti wa halmashauri na makatibu wa mikoa mbalimbali nchini.
Alisema kuna umuhimu wa viongozi hao kuielimisha jamii umuhimu wa kufanya kazi na kujishughulisha katika kutafuta riziki halali na kuachana na tabia ya kutafuta kwa njia ya dhuluma kwa kuwa hata Mungu hapendi.
“Kauli ya Rais inasema ‘Hapa Kazi Tu’ tunatakiwa kuisimamia kwa kuwajibika na kuitekeleza. Tujitume katika ajira zetu na biashara ili tupate riziki ya halali katika njia zinazompendeza Mwenyezi Mungu,” alisema Sheikh Zuberi.
Katika hatua nyingine, Mufti aliwataka viongozi hao kujenga umoja, mshikamano na kusahau hitilafu walizonazo. Pia waangalie namna ya kutatua changamoto mbalimbali zilizopo. “Nyumba ni moja tunayojenga hivyo haina haja ya sisi viongozi na waumini wetu kugombea fito, tutambue kuwa sisi kama viongozi tuna jukumu la kuwajenga waumini ili wawe na tabia njema za uadilifu maana uadilifu umepotea miongoni mwetu,” alisema.
Aidha, Mufti alizungumzia suala la dawa za kulevya na alisema elimu zaidi inatakiwa kwa jamii na hasa vijana kwa kuwa ndio waathirika wakubwa. Mufti Zuberi pia aliwataka waumini wote wa dini hiyo kuwa wazalendo na kuipenda nchi, huku akihimiza viongozi kutumia majukwaa vizuri kwa kuhamasisha upendo na mshikamano ili kuendeleza amani iliyopo.
Semina hiyo ya kwanza kufanyika, iliambatana na mada mbalimbali zikiwamo utiifu kwa viongozi, utawala bora, uchumi na maendeleo, kubadilika kutoka kwenye ufanyaji kazi kwa mazoea pamoja na mambo mengine.