|
WIZARA ya Katiba na Sheria imeeleza hatua za kukomesha ucheleweshaji na usikilizaji wa kesi za jinai ; na kusema itakuwa ikitaka maelezo ya kisheria ya muda mahususi wa kumaliza kesi husika bila kisingizio cha upelelezi kutokamilika.
Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe alisema hayo jana wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake na kusisitiza kwamba hiyo ni hatua ya kutatua kero zinazokwamisha au kuchelewesha kesi hizo.
“Mazoea ya kila kesi ya jinai, iwe ndogo au kubwa kuruhusiwa muda mrefu wa upelelezi, hata kwa kesi ambayo mtuhumiwa kakiri kosa au mashahidi wapo walioshuhudia kosa likitendeka, sasa basi,” alisema Mwakyembe.
Hatua nyingine ya kutatua kero ya ukwamishaji wa upatikanaji wa haki sawa kwa wote imetajwa kuwa ni wizara hiyo sasa kuchukua hatua kali zaidi dhidi ya wale wote waliohusika na upotevu wa mafaili lengo likiwa ni kukomesha hali hiyo isirudiwe.
Dk Mwakyembe alisema upotevu wa mafaili ya kesi umezidi kila kukicha licha ya Mahakama kuchukua hatua stahili za kiutendaji na kinidhamu unapotokea, hali ambayo imekuwa ikisababisha mrundikano wa kesi mahakamani.
Vile vile alisema ubambikizwaji kesi katika vituo vya Polisi umekuwa ukijirudia mara nyinyi hali ambayo alisema katika mwaka wa fedha 2016/2017 itaangaliwa kwa jicho kali zaidi kuidhibiti.
“Wizara itatafuta njia muafaka ya kisheria kuhakikisha kuwa hali hiyo haijitokezi katika mfumo wetu wa haki jinai,” alifafanua.
Alisema Wizara ya Katiba itatumia kwa karibu zaidi Jukwaa la Haki Jinai chini ya Mkurugenzi wa Mashtaka; ambalo linajumuisha wakuu wa vyombo vyote vya haki jinai katika kutatua kero hizo zinazochelewesha au kukwamisha upatikanaji wa haki sawa kwa wote.
Akizungumzia juu ya ucheleweshaji wa nakala za hukumu na mwenendo wa mashauri, alisema pamoja na jitihada bayana zinazofanywa na Mahakama kuongeza kasi katika utoaji wa nyaraka, wizara yake inaliona tatizo kuwa kubwa linalohitaji Mahakama kuongezewa kada ya wachapaji na vitendea kazi.
Akitaja vipaumbele vya wizara yake katika mwaka ujao wa fedha, Dk Mwakyembe alisema miongoni mwake ni pamoja na kufanya mapitio ya sheria za usafirishaji, uwekezaji na sheria zinazosimamia eneo la ustawi wa jamii linalojumuisha sheria tano.
Alitaja sheria hizo ni za maadili ya viongozi wa umma namba 13 ya mwaka 1995, sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa, sheria ya bima ya afya, sheria inayosimamia hifadhi ya jamii na mfumo wa sheria zinazosimamia elimu pamoja na sheria zinazosimamia biashara na uchumi.
Wakati huohuo sakata la mgawo wa fedha za akaunti ya Tegeta Escrow limeibuliwa tena bungeni na kambi ya upinzani ambayo imeitaka serikali kuweka wazi matokeo ya uchunguzi wa majaji wawili wa Mahakama Kuu wanaotuhumiwa kuhusika.
Msemaji wa Kambi ya Upinzani Bungeni wa Wizara ya Katiba na Sheria, Tundu Lissu, aliibua hoja hiyo jana. Majaji wanaotuhumiwa kupata mgawo wa fedha hizo ni Profesa Eudes Ruhangisa anayedaiwa kupatiwa Sh milioni 404.25 na Jaji Aloysis Mujulizi anayedaiwa kupatiwa Sh milioni 40.4.
Akichangia mjadala wa kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria ya mwaka wa fedha 2016/17 bungeni jana, Lissu alisema mwaka mmoja na nusu umepita tangu Bunge lipitishe tume ya uchunguzi ya kijaji kwa ajili ya kuchunguza tuhuma dhidi ya majaji hao.
Alisema Desemba 22, 2014, Rais mstaafu Jakaya Kikwete wakati akizungumza na wazee, alisema suala la majaji hao limepelekwa kwenye Tume ya Nidhamu ya Mahakama.
“Baadaye tukaambiwa kuwa uchunguzi dhidi ya majaji hao umekamilika, sasa huu ni mwaka mmoja na nusu tangu uchunguzi dhidi yao ufanyike, taarifa iko wapi?” Alihoji.
Alisema nidhamu kwenye Mahakama ni jambo la muhimu na kwamba tuhuma zinazowakabili majaji hao, zimeiaibisha tasnia nzima ya Mahakama. Lissu alitaka suala hilo liwekwe wazi, ikiwa ni pamoja na hatua walizochukuliwa.
Alisema yapo mazoea yaliyojengeka ya kuona mahakimu wakiadhibiwa lakini si majaji. Wakati huo huo, Lisu alihoji umri halali wa kustaafu kwa Jaji Mkuu, Mohamed Chande Othman kwa kusema majaji wenzake anaolingana nao umri wameshastaafu.
0 Comments