RAIS John Magufuli jana alikuwa kivutio kwa maelfu ya wananchi waliohudhuria sherehe za kuapishwa kwa Rais Yoweri Museveni wa Uganda.
Wananchi walilipuka kwa furaha baada kiongozi huyo wa Uganda kumtambulisha Rais Magufuli. Rais Museveni aliapishwa kuwa Rais wa Uganda kwa kipindi kingine cha miaka mitano katika halfa iliyohudhuriwa na viongozi wengi wa mataifa mbalimbali.

Tukio hilo lilirushwa moja kwa moja na vituo vya televisheni vya ndani ya nchi na vya kimataifa. Alipofika jukwaani, Rais Museveni alianza kuwatambulisha wakuu na marais wa nchi mbalimbali waliofika katika sherehe hiyo ikiwa ni muda mfupi tangu alipoapishwa.
Mara alipotaja jina la Rais Magufuli, umati ulirindima kwa makofi, shangwe na vigelegele, hatua iliyofuatiwa na Rais Magufuli kusimama na kuwapungia mkono wananchi hao.
Rais Magufuli ameibuka kuwa kiongozi maarufu katika nchi zinazounda Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), kutokana na hatua mbalimbali anazoendelea kuzichukua katika uendeshaji wa serikali yake, ikiwa ni pamoja na vita dhidi ya rushwa na ufisadi, tangu alipoingia madarakani mwishoni mwa mwaka jana.
Akiondoka katika Viwanja vya Uhuru vya Kololo ilipofanyika sherehe hiyo, waandishi wa habari walijaribu bila mafanikio kutaka kufanya naye mahojiano, lakini Rais Magufuli hakupata muda wa kutosha wa kuzungumza nao.
Akiwa amefuatana na ujumbe wa watu wachache, Rais Magufuli aliwasili nchini hapa Jumatano akitokea Arusha, akitumia ndege maalumu ya Rais.
Aliwasili Kampala ikiwa ni safari yake ya pili nje ya Tanzania, tangu alipoapishwa kushika wadhifa wa urais baada ya kushinda Uchaguzi Mkuu wa mwishoni mwa mwaka jana.
Safari yake ya kwanza ilikuwa ni katika nchi ya Rwanda. Mapema, Rais Museveni alisaini kiapo cha uaminifu ili kulitumikia taifa hilo kwa mara nyingine, na kukabidhiwa zana za kufanyia kazi na Jaji Mkuu wa Uganda, Bart Katureebe.
Wakuu na marais wa nchi mbalimbali waliohudhuria sherehe hizo, nchi zao zikiwa kwenye mabano ni: Rais Uhuru Kenyatta (Kenya), Rais Omar al-Bashir (Sudan), Rais Salva Kiir (Sudan Kusini), Rais Robert Mugabe (Zimbabwe), Rais Jacob Zuma (Afrika Kusini) na Rais Mahamadou Issoufou (Niger).
Pia marais wastaafu wa Tanzania Ali Hassan Mwinyi na Jakaya Kikwete walihudhuria. Marais wengine walioonekana kuvuta hisia za wananchi wengi na kushangiliwa kwa nguvu ni Kenyatta na Omar al-Bashir.
Akimtambulisha Rais Al-Bashir, Rais Museveni alisema Uganda imepuuza amri ya Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC) ya kutaka Rais Al-Bashir kukamatwa.
Alisema “ Tumeamua kupuuza agizo hilo kwa sababu awali wakati Mahakama hii inaundwa, tulidhani ilikuwa makini lakini baadaye tukagundua ipo kwa ajili ya watu wasio na hatia.” Rais Museveni aliibuka mshindi katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Februari mwaka huu kwa kupata asilimia 60.75 ya kura zote.
Alifuatiwa na mpinzani wake wa karibu, Dk Kizza Besigye wa Chama cha Forum for Democratic Change (FDC) aliyepata asilimia 35.37 ya kura, huku Waziri Mkuu wa zamani, Amama Mbabazi, ambaye alipinga mahakamani ushindi wa Rais Museveni na kushindwa katika kesi hiyo alipata kura asilimia 1.43.
Rais Museveni, ambaye ni Mwenyekiti wa Chama tawala cha NRM, amekuwa madarakani tangu mwaka 1986.